Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Mt. Basili Mkuu

Basili Mkuu

Mtakatifu Basili alistahili kuitwa 'Mkuu' kwa sababu ya akili na utakatifu wake. Alikuwa mtoto wa Mtakatifu Basili Mzee na Mt. Emilia. Alizaliwa Kaisarea katika mkoa wa Kapadokia (Uturuki) mwaka 330. Mtakatifu Makrina ndiye dada yake. Tena, Watakatifu Gregori wa Nisa na Petro wa Sabate ni ndugu zake. Alisoma katika mji wa Konstantinopoli (Uturuki) na katika Atene (Ugiriki). Pale Atene alipata rafiki mmoja ndiye Mt. Gregori wa Nazianze.

Walipendana sana. Walijibidisha kuendelea katika utakatifu na maarifa yote. Basili alikuwa fundi wa kutumia Lugha kifasaha, na kama angekuwa mpenda makuu, angeweza kuyapata hayo kwa watu. Lakini aliyapuuza yote hayo, akataka kusifiwa na Mungu tu.

Alipokuwa na wafuasi ambao walikusanyika na kuzunguka, alianzisha nyumba ya kitawa huko Asia Ndogo (Uturuki). Aliwaunganisha watawa na alitunga sheria ambazo zimeendelea kutumika kwa karne nyingi, mpaka leo zinatumika na watawa wa Kanisa wafuatao madhehebu ya Mashariki. Mtakatifu Basili aliishi maisha kamili ya kitawa kwa muda wa miaka mitano tu, lakini maongezi yake pamoja na maongezi ya Mt. Benedikto katika karne ya sita yalikuwa msingi wa maisha ya kitawa.

Mt. Basili alipata Upadirisho mwaka 363 na aliwekwa kuwa askofu wa kaisarea mwaka 370. Aliwapinga kabisa wazushi wafuasi wa Arios. Alitunga vitabu vingi vya mafundisho ya dini. Wakaisari walimwogopa sana, maana Basili hakuwa na hofu katika kuzitetea haki za Kanisa. Mungu mwenyewe alizuia adui zake wasimwue. Kaisari Valentini alipotaka kumfukuza Basili aende katika nchi nyingine, wakati wa kutia saini yake Kalamu yake ilivunjika ghafla. Ikaletwa nyingine, nayo ikavunjika. Ikaletwa ya tatu, vile vile ikavunjika. Mwisho alishikwa na hofu sana hivi kwamba hakudhubutu tena kumfukuza Basili katika utawala wake.

Askofu Basili alijitahidi sana kuhakikisha kama Mapadre wa jimbo lake walikuwa wanautekeleza vizuri wajibu wao. Pia, bila wasi wasi alikataa kabisa kumpadirisha yeyote ambaye, kwa maoni yake, hakufaa kuwa padre. Hivyo hali ya jimbo lake kuu ikawa mfano mzuri wa majimbo mengine mengi.

Mt. Basili hakuweza kukaa kimya alipotambua kwamba watu wenye cheo au matajiri walitenda kinyume cha wajibu wao wa Kikristo. Siku moja, alipopata nafasi ya kuwahubiria, alisema hivi: " Wakataa kutoa fedha kwa sababu, eti, fedha zako hazitoshi kwa mahitaji yako mwenyewe, lakini huku ulimi wako ukiomba radhi, mkono wako unakuhukumu; kwa maana ile pete ya kidoleni mwako yadhihirisha uongo wako. Nguo zako zilizo za ziada zingewatosha maskini wangapi? Nawe wadhubutu kumwondoa mtu maskini bila ya kumpa cho chote?"

Hata hivyo, Mt. Basili aliona kuwa wajibu wa kutoa msaada ulikuwa si wa matajiri tu; hata watu maskini walilazimika kutoa. Siku moja aliwaambia hivi: " Je, wewe u maskini? - Sawa- Lakini wapo walio maskini kupita wewe. Vile vichache ulivyo navyo wewe, vinakutosha kwa siku kumi, lakini alicho nacho maskini huyu hapa, kinamtosha kwa siku ya leo tu. Kwa hivyo, usiogope kuvitoa vichache ulivyo navyo. Usiiangalie faida yako mwenyewe kuliko mahitaji ya wengine. Umpe mwombaji asimamae mlangoni pako chakula chako cha mwisho, baada ya hapo utegemee wema wake Mungu".

Kazi nyingi nzito, Ugonjwa na kujinyima kwake vilimdhoofisha upesi Mt. Basili, hata akafariki mwenye umri wa miaka 49. Ilikuwa mnamo tarehe moja Januari 379.

Maoni


Ingia utoe maoni