Alhamisi. 25 Aprili. 2024

Mt. Ignasi wa Loyola

Ignasi wa Loyola

Inyasi wa Loyola

Padre na Mwanzilishi wa Kanisa

Inyasi alizaliwa mwaka 1491 huko Loyola (Hispania ya Kaskazini). Wazazi wake walikuwa matajiri, wakajaliwa kupata watoto kumi na mmoja, watatu wakiwa wa kike na wanane wakiume, Inyasi ndiye aliyekuwa kitinda mimba (Mtoto wa mwisho kuzaliwa). Katika ujana wake aliingia kazi ya uaskari, akapigana kwa uhodari na maadui wa nchi yake. Walipokuwa karibu kuteka mji wa Pampeluna, alipigwa risasi mguuni. Akapaswa kulala kitandani kwa siku nyingi ili mguu wake upate kupona. Aliudhika sana kwa maana hakuwa na kitu chochote cha kufanya hapo kitandani kutwa kucha. Mwishowe aliomba kitabu cha kusoma, akapewa vitabu vya Maisha ya Yesu na Maisha ya Watakatifu. Baada ya muda alipata kutambua kwamba ujasiri wa kweli unapatikana katika kuufuata mfano wa watakatifu kuliko katika ushujaa wa kijeshi. Nia ya Inyasi sasa ilikuwa kumtumikia Yesu Mfalme.

Alianza kufikiri juu ya maisha yake kiroho. Mambo hayo yalichukua muda, wala hayakuendelea bila matatizo. Siku moja Bikira Maria alimtokea na mara mashaka yake yalikwisha. Alijitolea mwili na roho kwa Yesu akiapa kumtumikia mpaka kufa kwake, atakuwa askari wa Kristu, na kufuata matendo ya ujasiri ya watakatifu.

Inyasi alipopona alienda kanisa la Monte Serat akaungama dhambi zote alizotenda tangu kupata akili. Alivua mavazi ya kiaskari akautundika upanga wake kwenye altare ya Bikira Maria. Alijificha muda wa mwaka mzima pangoni mwa Manresa akisali na kufunga kutwa.

Hapo ndipo alipoandika kwa uongozi wa Bikira Maria kitabu kile bora kiitwacho "Mazoezi ya Kiroho". Watu wengi wamepata kuongoka na kupata utakatifu kwa kufuata mashauri yaliyoandikwa humo. Kisha kumaliza mafungo ya mwaka mzima huko Manresa, alienda kuhiji Yerusalemu. Aliporudi alijifunza muda wa miaka sita, akianza na sarufi ya kilatini kwenye shule ya wavulana ya Barselona (Hispania). Wakati ule Inyasi alikuwa na umri wa miaka 33.Baadaye alisoma teolojia katika Chuo Kikuu cha Paris (Ufaransa). Alipokuwa na umri wa miaka arobaini na saba, alipata upadre huko Roma (Italia), akamaliza mwaka mzima akijitayarisha kwa Misa yake ya kwanza

Huko Paris alikutana na Mtakatifu Fransisko Ksaveri na vijana wengine. Akiwa na hao vijana, Inyasi alianzisha shirika la Wajesuiti au "Chama cha Yesu". Wajesuiti hao waliweka nadhiri ya kwenda popote watakapotumwa na Baba Mtakatifu wa Roma. Walifaa sana kwa kustawisha dini Katoliki katika nchi zote. Hata siku hizi bado wanashindana na maadui wa Kanisa Katoliki kila mahali duniani. Ndiyo maana watu wabaya wanawachukia, hata pengine wanajaribu kuwafukuza. Mt. Inyasi na mapadre wa shirika lake huzoea kusema: "Tutende vitu vyote ili Mungu apate kusifiwa zaidi na zaidi."

Inyasi wa Loyola alifia huko Roma mwaka 1556. Pamoja na Fransisko Ksaveri aliandikwa katika orodha ya Watakatifu mwaka 1622.

Maoni

Filbert Mwacha

Tunaomba kwa kadiri Mungu atakavyo wajalia muweke historia za Watakatifu wote

Filbert Mwacha

Tunaomba kwa kadiri Mungu atakavyo wajalia muweke historia za Watakatifu wote

Mwanga Mashaka

"Tutende vitu vyote ili Mungu apate kusifiwa zaidi na zaidi."

Robert Michael Ntabo

Tutende vitu vyote ili Mungu apate kusifiwa zaidi na zaidi."

Ingia utoe maoni