Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Mei 10, 2019

Ijumaa, Mei 10, 2019,
Juma la 3 la Pasaka

Mdo 9:1-20;
Zab 117:1-2 (K. Mk 16:15);
Yn 6:52-59.


MAISHA YETU YANATOKA KWA KRISTO!
Mt. Paulo ambaye tunamsikia katika somo la kwanza la leo alikuwa mtu mwenye Elimu ya juu/ busara aliyesoma chini ya mwalimu mkuu Gamaliel. Uongofu wake wa ghafla ulitokea barabarani akielekea Dameski. Paulo ambaye alikuwa na mambo mengi, lakini akikosa jambo muhimu zaidi ambalo alilipata kupitia ndani ya tukio hili la wongofu. Alimpata Yesu Kristo. Baada ya uzoefu huo Paulo anatangaza, "Kwangu mimi, kuishi ni Kristo"; kama nilivyo, maisha ni Yesu Kristo" au "Naweza kufanya yote katika Yeye anitiaye nguvu." "Naishi sasa si kwa maisha yangu mwenyewe bali kwa maisha ya Kristo anayeishi ndani yangu."

Mara baada ya Paulo kukutana na Yesu, maisha yake hayakubaki kamwe jinsi yalivyo kuwa mwanzo. Alibadilika kabisa. Alikuwa kiumbe kipya katika Kristo. Nasi pia tunampokea Kristo katika Ekaristi Takatifu. Ni kwa kiasi gani Ekaristi inabadilisha maisha yetu? Ni kwa kiasi gani najitoa mwenyewe kwa Kristo pale anapojitoa mwenyewe kwangu?

Katika somo la Injili, Yesu anasema “msipo ula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake hamna uzima ndani yenu”. Wengi wao walichukizwa na kuanza kuuliza uliza juu ya maneno yake. Inavutia kwamba wakati Yesu anapokutana na maneno makali ya wengine, anajibu tena kwa ujasiri mkubwa zaidi na uwazi zaidi. Hili linamuonesha kuwa mtu wa ujasiri mkubwa, mwenye nguvu na kuelewa. Unafunua pia kwetu sisi ujasiri ambao sisi tunapaswa kuwa nao katika ulimwengu huu. Ulimwengu tunaoishi ni ulimwengu unao kataa ukweli. Unakataa ukweli wa maadili, lakini pia unapinga ukweli wa ndani wa kiroho pia. Ukweli huu wa ndani ni kama uwepo wa uzuri wa Ekaristi Takatifu, umuhimu wa sala za kila siku, unyenyekevu, na kumtegemea Mungu, kuweka mapenzi ya Mungu mbele kuliko kitu chochote nk. Tunapaswa kutambua kuwa kila mara tunapo sogea karibu zaidi na Mungu, ndivyo tunavyozidi kujikabidhi kwake zaidi, na tutakapo hubiri ukweli wa Mungu ndivyo tunavyo upa ulimwengu shinikizo uache kutuiba kutoka kwa Mungu.

Sasa tufanye nini? Tunajifunza kutoka katika ujasiri na nguvu ya Yesu. Tunapojikuta sisi wenyewe tukiwa katika changamoto au tunapo hisi kana kwamba Imani yetu inashambuliwa, ndivyo tunavyo takiwa tuzame ndani zaidi na kuwa waaminifu zaidi na zaidi. Hili litatufanya tuwe na nguvu zaidi na kufanya vishawishi vinayokuja kuwa nafasi ya neema! Chagua kuiga ujasiri na ushupavu wa Bwana wetu na utakuwa chombo chenye kuonekana cha neema na huruma.

Sala:
Bwana, ninaomba unipe ujasiri wa nguvu zako . Ninaomba unipe mwangaza katika utume wangu na unisaidie kukutumikia kiaminifu katika kila kitu. Ninaomba nisiwe muoga ninapo kutana na changamoto za maisha bali nitazame hamu yangu ya kukutumikia kwa moyo wangu wote. Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni