Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Mei 03, 2019

Ijumaa, Mei 3, 2019
Juma la 2 la Pasaka

Sikukuu ya Mitume Filipo na Yakobo, Mitume

1 Kor 15: 1-8;
Zab 18: 2-5;
Yn 14: 6-14


TUNAITWA KUWA VYOMBO VYA HABARI NJEMA!
Leo tunawakumbuka mitume wa Bwana, Filipo na Yakobo. Yakobo ana barua yake katika Agano Jipya. Baada ya ufufuko Yesu alimtokea Yakobo ambaye baadae alienda Yerusalemu na kuongoza Kanisa kwa muda Fulani, na baadae alipigwa kwa mawe na kufa shahidi.

Filipo ni mtume ambaye anatajwa katika ule muujiza wa kuongeza mikate katika Injili. Ni yeye aliyevuviwa kumbatiza ofisa wa Ethiopia katika kitabu cha matendo ya mitume. Mapokeo yanasema kwamba Filipo alihubiri Ugiriki, Frigia na Syria. Yeye pamoja na Mtakatifu Bartholomeo walisulubishwa miguu juu kichwa chini. Mapokeo yanatuambia kwamba Filipo aliendelea kuhubiri akiwa amefungwa pale msalabani miguu juu kichwa chini mpaka alipo kufa.

Yakobo na Filipo waliyatoa maisha yao kwa Kristo, bili kushikilia chochote. Lakini ilichukuwa muda kukua katika imani na ujasiri katika kumfuata Yesu. Wanatupa changamoto na sisi tukue kwa kujikabidhi kikamilifu kwa Yesu na kuamini kikamilifu mapenzi yake.

Ingawaje filipo na Yakobo hawakuwa watu waliojaa Imani mwanzoni. Yesu hakuwaacha aliwavuta tu kwake, sisi nasi Yesu hatatuacha kama tutaamua kujikabidhi kwake. Aliendelea kuwaita kwenye utakatifu na huduma takatifu, na ataendelea kufanya kwetu pia.

Sala:
Bwana, ninakushukuru kwa kutokuniacha mimi, hata pale ninapo tenda dhambi na kwenda mbali nawe. Nisaidie niweze kuvumilia katika Imani yangu kwako na niweze kujibu wito wako kwa kukufuata kikamilifu popote unapotaka kuniongoza.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni