Alhamisi, Aprili 18, 2019
Alhamisi, Aprili 18, 2019.
Juma Kuu
ALHAMISI KUU
Kut 12: 1-8,11-14;
Zab116: 12-13,15-18;
1 Kor: 11:23-26;
Yn 13: 1-15
FANYENI HIVI KWA KUNIKUMBUKA MIMI!
Leo tunaanza siku tatu, muhimu katika Pasaka-maadhimisho matatu makuu ya Imani yetu Katoliki. Leo tunaanza na zawadi ya Bwana wetu ya Ekaristi Takatifu tuliopewa kwa ukuhani aliosimika. Kesho tunaingia katika fumbo la Msalaba. Na Jumamosi jioni tunaingia katika utukufu wa ufufuko wake.
Alhamisi kuu jioni, tuna adhimisha siku ambayo Yesu aliweka Ekaristi Takatifu, kwa kusema “fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” Tangu siku hiyo Misa Takatifu imekuwa ikiadhimishwa mara nyingi sana katika kila pembe ya dunia kwa kutii amri ya Yesu.
Kama tungeelewa thamani na zawadi hii Takatifu, Ekaristi Takatifu! Ekaristi Takatifu ni Mungu mwenyewe katika ulimwengu huu, tuliopewa sisi kutugeuza na kutufanya tuwe tunachopokea. Ekaristi Takatifu katika ukweli halisi, inatubadilisha sisi tuwe kama Kristo mwenyewe. Tukipokea Ekaristi Takatifu tunavutwa kwenye maisha ya Kimungu ya Utatu Mtakatifu. Tunaungana na Mungu na tunapewa chakula cha uzima wa milele.
Yesu pia alioonesha mfano wa unyenyekevu wa hali ya juu na huduma ambayo tunapaswa kuitoa na kuiiga tunapo amua kumfuata na kuwa wamoja pamoja naye. Aliwaosha miguu mitume ili kuwafundisha wao na sisi kwamba mwili na damu yake tumepewa ili tuweze kupenda kama yeye alivyo penda. Ekaristi inatugeuza kuwa watumishi wa unyenyekevu wa kweli. Tunaitwa tuwahudumie ndugu zetu. Huduma hii inachukua hali mbali mbali lakini ndicho tulichoitiwa kufanya. Huduma katika unyenyekevu ni muonekano mzuri wa kueleza muunganiko wetu na Mwana wa Mungu. Ukuu unaonekana katika hali ya dunia kama kitu kizuri na cha kutamanika. Lakini leo Yesu anatupa aina nyingine ya ukuu. Alhamisi kuu, anaonesha kwamba ukuu huu katika unyenyekevu unapatikana katika huduma hii. Ili kumuiga yeye inatupasa kuacha majivuno yetu kwanza. Na hili linawezekana tunapopokea Ekaristi Takatifu tukiwa safi na wenye Imani. Ekaristi inatusaidia kuwapenda na kuwatumikia namna hii. Na kitendo hichi cha upendo na huduma kitashinda katika mioyo yetu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Tukiwa tuna adhimisha Alhamisi kuu, tunapata changamoto ya kuangalia unyenyekevu wetu, na kubadilika na kujikita katika kuwahudumia wengine.
Juu ya Msalaba, alitoa maisha yake kwasababu ya dhambi zetu na kutupatanisha na Baba. Lakini kifo chake msalabani haina maana kwamba tutakwenda Mbinguni moja kwa moja. Tunapaswa kushirikiana na neema yake aliotoa pale msalabani. Na hii ndio Ekaristi iliotoka ndani yake. Yesu aliyekufa juu ya Msalaba ndiye Yesu yule yule aliye aliye juu ya altare wakati wa misa. Ambaye alilipia dhambi zetu pale msalabani ndiye yule yule anaye tupa neema zake na ukombozi juu ya altare wakati wa misa. Juu ya Msalaba Yesu alitoa sadaka kamili ambayo haina haja ya kurudiwa tena. Katika altare sadaka ile ile ya Yesu alioitoa inawekwa wazi tena kwa ajili ya ukombozi wetu. Si kwamba inarudiwa tena bali ni sadaka ile ile ya Yesu alioitoa msalabani. Inawezekana je? Ni kwasababu Mungu hafungwi na sehemu wala wakati wala historia, ndio maana sadaka inakuwa ileile. Yeye anayafanya yaliotokea wakati ule yawe tena wazi juu ya altare. Kwahiyo juu ya altare anatupa tena nguvu ya kukabili madimbwi ya dhambi na kuingia katika uwepo wake katika hali kamili. Kwa hiyo, kilicho tokea pale msalabani ndicho kinacho tokea altareni.
Ndivyo Yesu alivyo jikita katika kuleta ufalme wake kwetu. Hivyo, tutakavyo kwenda kanisani leo, tuangalie kwa makini katika hostia Takatifu na kumuona Yesu akiwa mbele yetu. Na kumuona yeye akitupa huruma yake. Tumuone yeye akitoa upendo wake.
Sala:
Bwana, nisaidie niweze kuwaza jinsi ya kuwa mtumishi. Nisaidie niweze kuishi unyenyekevu huu kwa matendo yangu. Ninaomba zawadi ya mwili wako Mtakatifu na damu yako vinibadilishe niweze kuwa mtu yule ambaye unapenda niwe. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni