Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Machi 22, 2019

Ijumaa, Machi 22, 2019,
Juma la 2 la Kwaresima

Mwa 37:3-4, 12-13, 17-28;
Zab 105:16-21;
Mt 21:33-43, 45-46


UPENDO UNAOTESEKA
Katika njia nyingi, Yusufu alikuwa mwaminifu, alikuwa akilindwa katika upendo na kutendewa vyema na Baba yake. Lakini kutokuwa na hatia kulimweka mashakani mara pale alipowaambia ndugu zake kuhusu ndoto yake, na alipowaonyesha kanzu nzuri Baba yake aliyokuwa amempa. Baadaye, ingawa ndugu zake walimpiga na kumuuza utumwani, Yusufu hakuacha kuziishi amri za Mungu. Hata alipokuwa ameshtakiwa kwa uongo na kufungwa gerezani kwamba alijaribu kumwingilia mke wa bwana wake kwa nguvu, yeye aliendelea kuwa imara mbele ya Mungu. Wakati akiwa gerezani, uwezo wake wa kutafsiri ndoto ulimfikia Farao ambaye hatimaye alimweka huru na kumweka awe mkuu baada yake. Kama Yusufu alivyoamini kwamba, Mungu atamletea mema, Mungu alifanya hivyo kwa ajili yake na kuutenga uovu. Nasi pia, tusikubali kamwe kumuacha Mungu tunapokabiliana na magumu siku zote katika maisha yetu. Tumgeukia Mungu Baba yetu na kumwomba atupiganie.

Katika hali zote za kuchukiwa na kukataliwa kwa karne zote, kuna mmoja tu aliyesimama imara kuliko wengine wote. Kukataliwa kwa Mwana wa Mungu. Yesu hakuwa na kitu kingine isipokuwa upendo kamili moyoni mwake. Alipenda ubora wa kila aliyekutana naye. Na alikuwa tayari kumpa upendo yeyote aliyekuwa tayari kuupokea. Ingawaje wengi waliupokea lakini pia wengi waliukataa. Ni vizuri kutambua kuwa kukataliwa kwa Yesu kuliacha maumivu ya ndani na mateso. Ni wazi kwamba mateso ya Msalabani ndio yaliokuwa ya hali ya juu kabisa. Lakini kidonda alichohisi moyoni mwake kwa kukataliwa kilisababisha mateso makubwa. Kuteseka namna hii ilikuwa ni kitendo cha upendo, sio kitendo cha udhaifu. Yesu hakuteseka ndani kwasababu ya majivuno au kwasababu ya ubinafsi wake. Bali moyo wake uliumia kwasababu alipenda kutoka ndani. Na pale upendo huo ulipo kataliwa, ulimjaza yeye huzuni kuu (Mt 5:4).

Jaribu kufikiria kama Yesu ange amua kukata tamaa. Jaribu kufikiria, kama kipindi cha kukamatwa kwake Yesu angeita malaika kama jeshi kutoka mbinguni kumwokoa. Ingekuwaje kama angefanya kitendo hichi cha kufikirika “watu hawa hawastahili!”. Matokeo yake yangekuwa tusinge pokea zawadi ya ukombozi wa milele kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko. Mateso yasinge badilika kwenda kwenye upendo.

Yesu alijibu kwa mapendo kamili pale alipolia kwa sauti kuu “Baba, wasamehe, hawajui watendalo.” Kitendo hiki cha upendo katikati ya mateso yake na kukataliwa kwake kilimfanya awe “jiwe kuu la msingi” la Kanisa, na hivyo kuwa jiwe kuu la maisha mapya! Tunaitwa kuiga mapendo haya na kushiriki sio tu kwakusamehe, bali pia kutoa mapendo matakatifu ya huruma. Tukifanya hivyo, sisi pia tunakuwa jiwe la msingi la upendo na neema kwa wote wanao hitaji zaidi.

Sala:
Bwana, nisaidie mimi niweze kuwa jiwe la pembeni. Nisaidie mimi sio nisamehe tu kila mara ninapokosewa bali pia nitoe upendo na huruma kwao. Wewe ni Mungu na mfano kamili wa upendo huu. Ninaomba nishiriki katika upendo huu, nikilia kwa sauti kuu pamoja nawe “Baba wasamehe, hawajui watendalo”. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni