Jumapili, Februari 24, 2019
JUMAPILI, FEBRUARI 24, 2019.
DOMINIKA YA 7 YA MWAKA C WA KANISA
1 Sam 26: 2,7-9,11-13, 22-23;
Zab 103: 1-4, 8,10,12-13;
1 Kor 15: 45-49;
Lk 6: 27-38.
------------------------------------------------
WAPENDE ADUI ZAKO
Vijana wawili walikuwa wakitembea majina yao ni Smith na Joan wakakutana na kijana mwingine, Smith akamsalimia huyu kijana lakini chakushangaza huyu kijana alijibu kwa hasira sana na ukali mwingi. Smith yeye alimjibu kwa utulivu na kwa upole. Walipo ondoka Joani alimuuliza Smith kwanini yule kijana alikuwa mkali namna ile? Akamuuliza huwa daima anakufanyia hivyo? Smith akajibu akasema daima anaongea vibaya ila mimi namjibu vizuri. Joani akamuuliza sasa wewe unawezaje kuvumilia na hata hukasiriki wakati yeye anakujibu vibaya tena hali ya hasira? Smith alijibu hivi “kwasababu sitaki yeye awe kwangu kama rimoti yakunifanya nitende nisivyopenda”.
Haijalishi ni nanmna gani watu wanaweza kututenda vibaya, bado tunauwezo wakuwarudishie na kuwatendea Kikristo.
Katika somo la kwanza Sauli anamtafuta kijana Daudi anataka kumuua. Daudi anapata nafasi ambayo angeweza kumuua Sauli lakini hakufanya hivyo kwasababu anafahamu sio sahihi kuua mtu machoni pa Mungu. Katika somo la pili Paulo analinganisha Yesu na Adamu. Kwa njia ya Adamu tulipata maisha ulimwenguni. Kwa njia ya Yesu tunapata maisha ya Mbinguni. Katika somo la Injili Yesu anatuambia badala ya kuwatendea maadui wetu vibaya tunapaswa kuwatendea kwa huruma na kuwasamehe.
Baba mmoja alikuwa akiishi na mke wake. Alikuwa na mtoto mmoja wa kiume. Baba alikuwa na bustani yake ambayo alikuwa akiipenda sana. Bustani hi ilikuwa nyuma ya nyumba yao. Baba alijitahidi kuwafukuza wanyama wakali waliokuwa wakitoka msituni na kuja kula katika bustani yake. Mbweha alikuwa mnyama ambaye alikua akija pale. Yule mtoto, Wazazi walimweleza jinsi gani wanyama wa pari walivyo wakali na kwamba hapaswi kutengeneza nao urafiki kwani watamdhuru vibaya. Daima Baba alikasirika kwamba wanyama walikuwa wakija kuharibu bustani yake. Baba alinunua bunduki na daima alikuwa akiipiga hewani ili kuwafukuza wanyama mbali mbali akiwepo mbweha. Lakini cha ajabu yule mtoto wao alikuwa akiwapenda wanyama na alitaka kuanza kutenengeneza urafiki na wanyama hawa. Baba aliamua kuweka fensi kulinda bustani yake.
Yule mtoto wake alikuwa akitupa chakula nje ya fensi ili kuwakaribisha wanyama lakini alikuwa akifanya hivi kwa siri ili baba asijue. Siku moja baba aligundua na alikasirika sana. Akamkataza yule kijana wake. Lakini yule kijana alibuni mbinu mpya ya kuwapa chakula bila baba kuona, ilifikia mahali wale mbweha walikuwa marafiki na kuvutwa karibu kiasi ambacho walifikia hata kuchukua chakula mkononi mwa yule kijana. Baba alipoona alimwambia mtoto wake kwakweli nilikuwa ninakosea. Kumbe ningeweza kufanya kama wewe, badala ya kuwakimbiza kwa risasi, kumbe ningeweza kufanya kama wewe, wanyama hao wakabaki na amani na hata wakati mwingine walikuwa wakija na kukaa na yule kijana pembeni, wakatengeneza urafiki, badala ya kuwa wanyama adui wakawa wanyama rafiki.
Mara nyingi sisi wakristo tunajisikia vizuri tunapo acha kurudisha kisasi kwa majirani zetu. Lakini Yesu alituambia tufanye kitu zaidi, ni lazima tuwapende. Kumbe kazi ya kufanya ni kuwapenda, na sio kuwakwepa tu. Tunaweza kutambua kuwa hili kwa ubinadamu ni ngumu sana lakini tunaweza kujifunza kwa yule kijana katika mfano hapo juu. Licha ya tabia za wenzetu na hali yao ya ukali bado tunaweza kuwapenda na tusikubali waturithishwe chuki au uadui wao.
Kurudisha visasi hii ni hali ya kuongeza giza kwenye giza. Mara nyingi tunajenga ukuta kwa watu tusiowapenda tunatumia nguvu nyingi sana badala ya kutumia nguvu kidogo na kuwapenda. Chuki haiwezi kuondoa chuki badala yake tupendo waweza kuondoa chuki. Tuige tabia ya Yesu ya kuwapenda maadui na hata kuwaombea kama alivyofanya pale msalabani hasa pale wanapotutesa katika maisha. Tusiwe na tamaa ya kurudisha visasi.
Sala:
Bwana, nisaidie mimi niweze kuwasamehe wale wote walinikosea. Niweke huru nisiwe muhukumu wa watu na nakuomba tabia hii uijaze huruma yako. Ninakuomba niweze kuiga huruma yako kamili katika maisha yangu. Yesu nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni