Ijumaa, Februari 22, 2019
Ijumaa, Februari 22, 2019
Juma la 7 la Mwaka wa Kanisa
SIKUKUU YA UKULU WA MT. PETRO (MTUME)
1 Pt 5: 1-4;
Zab 23: 1-6;
Mt 16: 13-19.
MAMLAKA YA KUTUMIKIA.
Petro alimuungama Kristo na kumkiri tena baada ya mateso na ufufuko wake. Sisi nasi tunapaswa kumkiri Kristo na kuishi daima, tukianguka katika dhambi daima tujue kimbilio letu ni Kristo.
Leo tunasherekea sherehe ya pekee kidogo: Kiti cha ukuu cha mtakatifu Petro (mtume). Hii sherehe sio kwaajili ya kumheshimu mtu binafsi kama ilivyo kawaida, sio tukio kama yalivyo mengine, bali ni Kiti cha ukuu. Si kwamba tunasherekea sherehe ya kiti kilichotengenezwa, bali ni kiti kama ilivyo “mwenyekiti” nafasi, mamlaka au ofisi. Leo tunasherekea kuwekwa kwa nafasi ya mamlaka ya Kanisa. Yesu Kristo ni kichwa cha Kanisa, ofisi hii haiondoi mamlaka yake kama kuhani mkuu na mfalme. Mungu amependa kutuchagua wanadamu, katika nafasi ya heshima ili atushirikishe neema yake.
Petro alimuungama Yesu, kwamba “wewe ndiwe Kristo mwana wa Mungu aliye juu” baada ya ungamo hili Yesu anamuita kwajina la Kefa, lenye maana kwa Kigiriki ya Petro. Yesu anampa Petro nafasi ya pekee kabisa kati ya mitume. Alikuwa ni mmoja wapo kati ya wale watatu waliokuwa na bahati ya kuona matukio ya pekee ya Yesu, kama vile kugeuka sura kwa Yesu na mateso ya Yesu akiwa bustanini Gestemane. Alikuwa ni mtume pekee aliyetokewa na Yesu siku ya kwanza tuu ya ufufuko wake. Petro pia aliongea kwaniaba ya mitume wengine, alikuwa wa kwanza kutoa jibu, mara nyingi hakuona shida kuongea ndio maana Yesu alimuonya wakati mwingine.
Kanisa kwa miaka yake 2000 ya historia kumekuwa na matukio ya neema na furaha, kumekuwapo changamoto za migogoro, Kipindi cha giza na mwanga. Lakini ukweli ambao haupingiki ni kwamba Kanisa limemudu na kuonesha kwamba Baba mtakatifu (wakili wa Petro) alipata mamlaka yake kutoka kwa Kristo na kwamba Roho wa Kristo yupo katika Kanisa hata leo na analiogoza.
Sala:
Bwana, tunakushukuru kwa zawadi ya Baba mtakatifu, tunakuomba umuongoze aendelee kutumia mamlaka yaliyotoka kwako katika kuwahudumia watu wote. Tunamuombea Baba Mtakatifu Fransisko na Maaskofu waliopewa mamlaka ya kufundisha ujumbe wa habari njema. Tunakuomba uwalinde na uwe nao na kuwapatia nguvu daima , waendelee kutuongoza kama Wachungaji wako katika kuelekea kwenye ufalme wako. Yesu tunakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni