Jumatatu, Februari 18, 2019
Jumatatu, Februari 18 2019
Juma la 6 la Mwaka wa Kanisa
Mwa 4: 1-15, 25;
Zab 50: 1, 8, 16-17;
Mk 8: 11-13
MIUJIZA KUTOKA MBINGUNI!
Katikati ya safari mbili (Mk 8:10 na 8:13), Marko anaeleza Yesu akikutana na Mafarisayo wakimwambia awape ishara kutoka mbinguni ambayo inadhihirisha kuwa anachofanya kimetoka kwa Mungu. Ukitegemea miujiza mingi ambayo Yesu alikuwa ameshafanya inashangaza bado Mafarisayo wanataka miujiza mingine. Wanachotaka Mafarisayo sio uponyaji mwingine, wala sio kutoa pepo, wala kuwalisha watu elfu nne, au dhoruba kumtii bali wanataka “ishara kutoka mbinguni” ambayo ni ishara ya ufunuo ambayo itawahakikishia bila kuwa na wasi wasi kwamba Yesu ana kibali cha Mungu.
Yesu anawakatalia kutimiza ishara waliouliza na anawaacha wakiwa wamesimama na kupakia mashua na kwenda ngambo nyingine ya bahari. Ni hakika kuondoka kwake ni alama ya kuto kupendezwa na mitizamo ya Mafarisayo. Sisi pia mara nyingi tumekuwa watu wakutaka ishara kutoka kwa Mungu, tunasahau ishara ya upendo wa Mungu anaotupa sisi kila siku katika maisha yetu. Imani yetu ndogo iliojazwa na akili na majivuno inatufunga tushindwe kuona miujiza mingi anayotenda Mungu katika maisha yetu. Imani yetu inatudai tubaki tukiwa waaminifu na wazi kwa Mungu, kwani anafunua Upendo wake katika udogo na unyenyenkevu.
Ni mara chache sana tunaweza kufikiria juu ya upendo wa Yesu kwa Mafarisayo. Mara nyingi, tunamfikiria akiwa mkali na kuwalaumu. Lakini kila neno alilokuwa akiwaambia likiwa kali lililenga kuwabadilisha wabadilike, alifanya hivyo kwasababu ya upendo wake. Ilikuwa ni jitihada yake ya kuwatoa katika hali ya tofauti na kuwaleta kwenye neema walio ikataa. Tutafakari, je sisi tupo kama Mafarisayo wanao kataa zawadi ya upendo wa Mungu anayotoa Yesu?
Sala:
Bwana, nisaidie nikupende kwa moyo mkunjufu na upendo mtakatifu. Nisaidie niweze kujuta juu ya dhambi zangu na dhambi za wengine. Nisadie majuto hayo yaweze kunifanya niwe na upendo zaidi na zaidi. Yesu nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni