Jumapili, Februari 17, 2019
“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Februari 17, 2019.
DOMINIKA YA 6 YA MWAKA C WA KANISA
Yer 17:5-8;
Zab 1: 1-4, 6;
1 Kor 15: 12, 16-20;
Lk 6: 17, 20-26.
------------------------------------------------
HERI ZA YESU: KINYUME NA MTAZAMO WA ULIMENGU
Wakati ukiwa tajiri au ukiwa na jina au ukiwa kiongozi wa kundi fulani, wewe hujakandamizwa. Ukiwa kwenye shida ukiwa mtu wa namna hii, ni simu tuu unapiga na mambo yote yanakuwa salama. Lakini ukiwa hauna marafiki na tena ukute wewe ni mgeni katika nchi fulani na tena unateseka na lugha, ni rahisi kuteseka kwani huna msaada sana. Hili ni kweli pia kwa wagonjwa, vilema, vipofu na wale wote wasiokuwa na sauti. Kuna wengi wasiokuwa na kazi, wanaokosa ulinzi, wanaoishi chini ya kiwango, wakiishi kila siku katika hali ya kutisha. Kila mmoja wetu ameshakutana nao. Wapo kati yetu. Hawa watu wanakumbana na heri hizi zaidi katika hali ya nafsi zao. Heri hizi zinaogopesha wakati unapoanza kuziishi walisemea baadhi ya watu wa zamani.
Katika somo la kwanza kutoka katika kitabu cha nabii Yeremia, tunasikia kwamba ole wao wanaomtegemea mwanadamu kwani maisha yao ni kama mti ulioota katika jangwa. Wakati wale wanaomtegemea Mungu maisha yao ni kama ule mti uliopandwa karibu na mto wa maji. Katika somo la pili tunaona kwamba ufufuko wa Yesu ndipo palipo lala matumaini yetu na Imani yetu. Na somo la Injili linaonesha Luka akizileta heri, tofauti na Mathayo mwenye heri tisa, Luka ana “heri” nne na “ole” zinazofuatana.
Yesu alikutana na watu wenye namna yao ya maisha waliojali maisha ya ulimwengu huu kuwa kitu cha thamani sana, kuwa na hela nyingi, anasa, umaarufu, mamlaka nk. Na hapa Yesu anawaambia wachukue hali yake ya umaskini wa roho, moyo safi, uwezo wa kuonesha huruma, kuteseka kwa ajili ya haki…). Uhuru huu wa kuchagua umewekwa kwa hali ya kuchagua kati ya mawili. Wengi watajikwaa kwa hili.
Kuna mfano mmoja, kuna familia moja ambayo iliishi maisha ya juu kabisa. Ambao mambo kama kutembea na kuchukua basi kwao kilikuwa ni kitendo kisichojulikana kwao. Kila sehemu aliotumwa kwa kazi walikuta nyumba nzuri ya kisasa ikiwasubiri pamoja na gari la kifahari. Walivyoishi waliishi kwa falsafa ya kwamba hapa duniani unaishi mara moja tu. Walikula katika hoteli za kifahari, kila aina ya tunda, chakula na kutembelea kila aina ya fukwe za bahari walipita.
Kwa miaka sita waliishi hivi. Kipindi hiki watu walikuwa wakiteseka katika mitaa yao, watu walipata vita na njaa kali, wengine walizikwa kiholela na wengine kuishi katika mateso makubwa. Lakini kwa familia hii mambo haya yalikuwa ni mambo yanayowapata wengine na wala hawakuguswa nayo.
Muda sio muda baba aliingia kwenye nyumba ya Bibi yake ambaye alikuwa amempatia kijitabu kidogo ambacho hakikuwa kisafi sana. Yeye aliamua kukisoma. Alikuta sehemu ikimwalika, awe na huruma, yeye alishangaa kwani shuleni alifundishwa kuwa na huruma ni jambo la aibu. Akakuta pia sehemu inayomwalika kukaa pamoja na maskini, yeye akashangaa kwamba alifundishwa akikaa na maskini watamletea shida zao na hivyo watamnyonya atabaki maskini. Kuanzia pale alianza kuishi hizi jumbe kutoka kwenye kitabu cha bibi yake. Alijikuta akikaa na watu, majirani na kuongea nao na kubadilishana mawazo, alijisikia kana kwamba ametoka katika ulimwengu mwingine. Mke wake hakumuelewa lakini baada ya muda naye aliliona ni jambo nzuri. Wakabadili ile falsafa ya maisha yao. Kwamba unaishi mara moja tuu, wakasema ndio unaishi mara moja lakini unapaswa kuishi na watu.
Kipindi fulani daktari mmoja ambaye alimtibu mama yake wakati akiwa mgonjwa alitumwa kwenda nchi ya jirani lakini daktari huyu walimtuma maksudi na kumwekea mtego ili endapo atatoa siri yeyote kwenye nchi ambayo anaenda kuhusu dawa fulani ambayo yeye aliifahamu jinsi ya kutengeneza basi angeuwawa. Huyu Baba kwasababu ya kuwa na nafasi katika serekali alishindwa kujizuia akaamua kumpigia simu yule Daktari kumjulisha kwamba asifanye hivyo, lakini serikali yake iliweza kunasa ile simu. Hapo yule baba akafukuzwa kazi na kupelekwa mahakamani na maisha yake yakaishia mahamani. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki.
Ni wangapi kati yetu kama wa Kristo tunaweza kusema tunaishi kwa thamani ya heri. Yapo mambo mengi yanayotusumbua mno, magari, maisha ya watoto wetu baadae, kuwa na nyumba nzuri, na mengine mengi. Yesu anawapa wafuasi wake namna mpya yakuchukulia mambo ulimwenguni. Haya yanaenda kinyume kabisa na mapigo ya ulimwengu. Kuingia katika ulimwengu wa heri, lazima kujinyima, tunahitaji kuamka kiroho. Utajiri na hali ya kuwa na mali nyingi inatuacha katika jangwa kubwa la kiroho. Bila Mungu hamu yetu ya kiroho haiwezi kutimizwa.
Sala:
Bwana, ninakuomba unifanye Mtakatifu. Ninakuomba unifanye macho yangu yakutazame wewe kwakupitia heri zako. Ninakuomba nisiishi maisha ya katikati au uvuguvugu. Ninakuomba niupigania utakatifu ili niweze kukufanya wewe kuwa kiini cha maisha yangu. Yesu nakutumaini a wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni