Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Januari 30, 2019

Jumatano, Januari 30, 2019,
Juma la 3 la Mwaka wa Kanisa

Ebr 10:11-18
Zab 110:1-4
Mk 4:1-20


Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza linatueleza juu ya ukuu wa ukuhani wa Kristo. Zaburi yetu ya wimbo wa katikati inatuambia kwamba yeye ni kuhani milele kufuatana na ukuhani wa Melkisedeki. Ukuhani wa Melkisedeki ni mkuu kuliko wa taifa la Israeli, Baba wa taifa la Israeli yaani Abraham alikwenda kwa Melkisedeki na kunyenyekea na kuomba Baraka.

Hivyo hakuna mzao wa Abrahamu aliyekuwa na ukuhani ulioweza kumfikia Melkisedeki, wazao wote wa Abrahamu wanapaswa kwenda kwa Melkisedeki na kubarikiwa. Ukuhani wa Yesu ni wa Kimelkisedeki: ni wa Milele na ni mkuu kuliko wa wana wote wa Abrahamu, hivyo wana wote wa Abrahamu ni lazima waende kwake kupewa baraka. Na pia sadaka aitoayo yeye huondoa dhambi zote, damu yake ina thamani kubwa kwani ni damu ya Mungu inayomwagika na hivyo huondoa dhambi kwa ubora kabisa.

Yote haya yaonesha ukuu na ubora wa Kristo. Kristo ameshakuja, ya zamani tuyaache. Ukuu wa damu yake utuongezee imani na kumpokea na kumwabudu zaidi. Tujifunike na damu ya Yesu, afunike kazi zetu, na kwa namna ya pekee afunike na afya zetu.

Afya zetu zipo hatarini kutokana na ueneaji wa sumu katika udongo, hewa, mimea, na vyakula. Vyote hivi vinaiweka afya zetu hatarini, pia teknologia inavyoongezeka imesababisha wakati mwingine afya zetu kuzorota. Magonjwa yanaongezeka kila siku, tuzifunike afya zetu kwa damu ya Yesu.

Katika injili, Yesu anatumia mfano wa mpanzi kuelezea mioyo mbalimbali inayopokea neno lake. Mioyo hubarikiwa kwa kadiri ilivyojifunua kuupokea ujumbe wa Mungu. Mioyo iliyojifunga ilishindwa kufaidi utajiri wa neno la Mungu. Tuache kuwa wachoyo kwa neno la Mungu-uchoyo kwa Mungu unatukosesha mengi. Ulimkosesha Solomoni ufalme katika nyumba yake, baada ya kufa kwake, familia ya Daudi ilipoteza makabila kumi.

Wengi wetu tuna hali mbaya kwa sababu ya uchoyo kwa Mungu. Tunajitetea mno kwamba sisi ni maskini, hatuna cha kumpa Mungu-na kumbe ni uchoyo tu. Sisi tuache uchoyo na hakika Bwana atatubariki zaidi. Tumsifu Yesu Kristo

Sala:
Ee Mungu ninakuomba Neno la Mwanao lizame ndani ya moyo wangu lizae matunda ya upendo, Amani, furaha na utulivu wa kuungana nawe na pia niweze kuwaleta wengine kwako kutokana na matunda yake. Yesu nakutumaini .
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni