Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Januari 27, 2019

Jumapili, 27/01/ 2019.
Juma la 3 la mwaka

Neh 8: 2-10;
Zab 19: 7-9, 14;
1 Kor 12: 12-30;
Lk 1: 1-4; 4: 14-21.
------------------------------------------------

TUMEITWA KUWA ROHO NA UZIMA!

Wakati Raisi anapoapishwa au waziri mkuu anapoapishwa, siku hiyo hutoa hotuba na tena hutoa mipango yake aliyojiwekea. Hili ndilo alilolifanya Yesu alipoingia katika Sinagogi na kusoma maandiko kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Alichagua sehemu hiyo kwasababu inafanya ufupisho wa utume wake wote. Ufupisho wake waweza kuwa hivi,: Habari njema kwa maskini na walioonewa.

Katika nchi moja ambapo mkate ulikuwa ni chakula kikuu. Ngano ilikosekana kwa muda, kwasababu ya ukame. Maskini walipatwa na njaa kali. Mfalme ambaye alikuwa aliwajali sana watu wake aliamua kusafiri na kwenda nchi za njee kwenda kutafuta mikate kwa ajili ya watu wake.

Njaa iliwakumba sana watu maskini zaidi kuliko wengine. Matajiri nao waliteseka njaa lakini sio sana kama maskini. Watu walikufa wengi sana. Matajiri walikuwa na pesa nyingi walinunua mkate kutoka njee lakini mkate ule ulikuwa hauna ladha na hata hivyo haukufaa kutunzwa kwa muda mrefu. Matajiri walikula lakini walijikuta wakidhoofika kila siku.

Nchi ilitanda simanzi kwani hali ilikuwa mbaya. Maskini walikuwa wamemwekea mfalme matumaini yao yote. Lakini walikuwa wakijiuliza mbona amechelewa kwa muda mrefu namna hii. Siku moja mjumbe wa mfalme akaingia katika mji nakusema: “furahi, nimekuja na habari njema kwa watu wote” watu wakajiuliza habari njema? Inamanisha mkate upo njiani unakuja?

‘Ndio rafiki. Mfalme yupo njiani anakuja na mikate mingi isiyohesabika. Watu walianza kucheza ngoma na kufurahi sana. Waliofurahi sana ni maskini lakini matajiri walifurahi kwa kiasi tu. Mmoja alisema kwamba amemsikia mjumbe wa mfalme akisema kwamba mkate utakuwa ni bure bila fedha. Wengine wakasema lazima ataweka kiasi fulani cha fedha hawezi kufanya bure. Haiwezekani. Wakamuuliza yule mjumbe je, mkate tutalipia au utakuwa bure, akasema kwa hakika utakuwa bure. Tazama mfalme akatokea akaja na mikate lakini chakushangaza akaanza kuwapa maskini bure. Matajiri wakashangaa kwamba hakuanza nao wakati wao ndio watu wakwanza kumpatia kodi katika ufalme wake. Wakamuuliza kwanini kuanza na maskini? Yeye akawajibu na kusema kwamba hawa wanauhitaji zaidi kuliko wengine.

Ni muhimu kulipata hili kwa hakika. Kwanza kabisa ni kwamba Injili ni habari njema. Ni habari njema kwa kila mmoja ila ni habari njema mara mbili zaidi kwa maskini. Maskini ni wapi hao? Ni wale wanaotambua hali yao ya dhambi, wanaoteseka na kupata kiu ya huruma ya Mungu. Watapata katika wingi kabisa. Sio kwamba mmoja anastahili au la bali kulipokea hili ni kwanjia ya neema na wema wa Mungu. Hili kwa mafarisayo lilikuwa kitendawili kwani wao walijiona kwamba wanauwezo wakujipatia utakatifu wao wenyewe, na kwamba Mungu yupo tuu kwa lengo fulani: kuhukumu wema wa mtu.

Maskini ni wale walio na mateso weliojeruhiwa na maisha, vipofu, wanaoteswa, mateka na wale wanaosubiri uhuru wa Mungu. Yesu hakuja ili awatafute wale wenye mali na wale wenye nguvu. Hakuna uhuru kwa wale waoishi kwa majivuno na kujihalalishia utakatifu wao wenyewe, wasioona dhambi zao na kuzikiri ili wakombolewe. Na wala hakuna uhuru kwa wale waliojikita katika madaraka na mali, wakidhani wanathamani kuliko wengine. “heri maskini wa roho kwa maana ufalme wa mbingu ni wao”. (Lk 6.20).

Liturjia ya leo inatualika leo tuadhimishe tukiwa na uzima na roho wa Mungu. Somo la kwanza na injili linatangaza uhuru wa wana wa Mungu. Hasa wale walio wagonjwa, walioonewa na maskini. Neno la uzima la Mungu linakuwa ndiyo furaha yao na linawafanya huru. Katika somo la pili tunatambua kwamba baada ya kujazwa roho tunapewa vipaji tofautofauti ili tuweze kuzaa matunda sisi kwa sisi na kujenga jumuiya ya Kikristo.

Mt. Paulo katika somo lake kwa wakorintho anatupatia lengo, “kuwa roho na uzima” kwa wote. Tunaitwa kuwa injili kwa majirani zetu. Neno wa Mungu amekuja kwetu na akakaa kwetu kwa njia ya ubatizo, hatujaachwa lakini tumekusanywa na kuwa mwili mmoja. Tunapowaona wale waliodhaifu tuwape matumaini kwani wao ni sehemu ya mwili mmoja wa Kristo. Sisi tumechaguliwa kila mmoja kwa sehemu yake, mitume, walimu, wafuasi nk.

Yesu kama Ezra kuhani, anatuonesha ni kwa jinsi gani neno la Mungu linaweza kuingia katika maisha yetu. Tunapaswa kushiriki moja kwa moja katika kulisikiliza neno la Mungu na pia katika liturjia ya Ekaristi. Liturjia hizi tukizishiriki vizuri zinakuwa sababu ya chanzo cha neema kwa familia zetu, marafiki na wote waliokaribu nasi.

Sala:
Bwana Yesu, neno lako ni kweli ni roho na uzima ninakuomba niweze kuwa chombo chako na hasa kwa wale wanaokuhitaji zaidi. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni