Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Disemba 23, 2018

JUMAPILI, DESEMBA 23, 2018.
------------------------------------------------
DOMINIKA YA 4 YA MAJILIO

Somo la 1: Mika 5:2-5 Yerusalem ilikuwa katika hali mbaya na utawala wa ukoo wa Daudi ulikuwa katika hatari ya kupotea. Nabii anatoa taarifa kwamba ukombozi utatokea, Betlehemu. Kutoka pale kiongozi mkuu atatokea pale na kuwaunganisha wote waliotawanyika na wale walio mateka.

Wimbo wa katikati Zab 80:2-3, 15-16, 18- mkono wako uwe juu ya yule uliyemchagua, yule uliyempa nguvu. Na hatutakuasi tena; tupe maisha ili tulitegemee jina lako daima. Mungu uturudishe utuangazie uso wako nasi tutaokoka.

Somo la 2: Ebr 10:5-10 Sadaka ya sheria ya Musa haikuweza kutakasa watu kutoka katika dhambi. Ni kwa njia ya Yesu, kwa njia ya utii wake na sadaka yake mwenyewe aliweza kuleta upatanisho kati ya Mungu na watu.

Injili: Lk 1: 39-45 Maria anamtembelea Elizabeth. Akiwa amejazwa na Roho Mtakatifu, Elizabeth anamsifu Maria na pia anatambua kwamba Maria amembeba Mwokozi wa Ulimwengu.
------------------------------------------------

KUFANYA MIOYO YETU SEHEMU YA MUNGU KUKAA

Majilio inaishilia na Masiha tunayemsubiri yupo mlangoni sasa anakaribia. Masiha yupo njiani anataka kuingia katika mioyo yetu. Kanisa linatualika leo ikiwa imebaki siku moja kabla ya Noeli tumuabudu Bwana. Kuanzia siku ile ya kwanza Mwanadamu alivyo kimbia mbali na Mungu kwa njia ya dhambi, Mungu alitangaza kuanza kumkomboa Mwanadamu. Na kumrudisha kwake. Na kumleta Yesu duniani alihitaji sehemu ya kukaa, tabenaklo.

Katika somo la kwanza nabii Mika analeta matumaini kwa watu wa Israeli. Kwamba Israeli kabila dogo na kataifa kadogo litanyanyuliwa. Kutoka katika mji wake mdogo Betlehemu, katika sehemu ya Daudi, mfalme mkuu atatokea. Kutoka katika sehemu ndogo kabisa kutatokea ufunuo wa utukufu wa Mungu. Huyu mfalme wa ajbu ataleta Amani na umoja kati ya mataifa.

Katika Injili ni kukutana kwa wanawake wawili wenye Imani. Maria na Elizabeth wanabidi wapitie hali fulani katika maisha yao. Wote walikuwa wamebeba siri ya ufunuo wa Mungu, katika kuleta huyu mfalme wa utukufu ambaye Mika anamtabiri. Ni wao wenyewe walioweza kuelewa furaha waliokuwa nayo ndani ya mioyo yao na ndani ya tumbo lao. Injili inaonyesha ujumbe wa Mungu kwa mwanadamua na jinsi mwanadamu anavyopaswa kujibu ujumbe huu.

Mungu alimchagua mwanamke wa kawaida tena wa kijijini, Maria kutimiza mpango wake kwa mwanadamu. Alikuwa ndiyo nyumba ambayo Mungu atakaa ndani yake. Ili Maria kumpokea Yesu ndani ya tumbo lake, alipaswa kumpokea kwanza ndani ya moyo wake. Kwa miezi tisa alipaswa kuishi ndani ya tumbo lake kama vile amri za Mungu ndani ya sanduku la Agano. Baada ya kutambua mpango wa Mungu Maria alijitoa kwa moyo wote bila kujibakiza. Maria anashika njia na kwenda kumsalimia Elizabeth, kushirikisha furaha yake. Elizabeth alikuwa amesubiria ahadi ya Mungu kwa miaka mingi. Kukutana kwao lazima kilikuwa ni kitendo cha furaha kubwa. Upendo alioubeba Maria ulimbariki Elizabeth na hapo akajazwa na Roho Mtakatifu. Elizabeth hawezi kuzuia furaha hii, anapaza sauti kwa furaha kwamba inakuwaje, Mama wa Mkombozi wake aende kumtembelea yeye? Wote wanajazwa furaha na wote wawili wanasubiria ahadi ya ukombozi.

Ujio wa mtoto Yesu ni wakati wa furaha katika familia. Kulikuwa na muda wa kusubiri, na muda wa kujiandaa na mwishowe kuzaliwa. Hivyo Noeli ni kipindi ambacho kinakuja kwa kufuatiwa na muda wa kusubiri, kujiandaa na baadae kuzaliwa kwa Kristo katika mioyo ya kila Mkristo. Tujiulize je na sisi tumejawa furaha na kusibiria ukombozi kama Maria na Elizabeth?

Njia pekee ya kuonesha kwamba tumemkubali ni kuwa wazi na kuwakaribisha wengine-kwa yeyote hasa kwa maskini na walio wapweke. Kuna mfano mmoja, kijana mmoja alikuwa anaitwa Martin, aliota kwamba Yesu atakuja kumtembelea. Siku zote alisubiria na kuendelea na shughuli zake. Katika kusubiria akawa amewapa baadhi ya maskini chakula, akawapa nguo baadhi ya maskini waliokuwa katika hali mbaya, mwingine alikuwa amemkosea akamsamehe. Siku nyingine akapatwa tena na ndoto, akaona Yesu anamuuliza, Je, Martini uliona nilivyokuja akasema hapana. Akamwambia nilikuja kwa njia ya wale uliowasaidia-yeyote uliowatendea walio wadogo hawa umenitendea mimi. Sio siku ya Krismasi tu Yesu anakuja na kubisha hodi katika mioyo yetu, anakuja kila siku na katika kila mwaka kwa ndugu zetu wote.

Neno alifanyika mwili akakaa kwetu. Huu ni ujumbe uliojificha kwa miaka mingi lakini sasa umefunuliwa na kufanywa ujulikane kwa watu wa amataifa yote ili waamini na kutii. Mungu amekuwa akitimiza kazi yake ya ukombozi tangu miaka mingi. Katika kipindi hiki cha Noeli tumruhusu atukomboe. Noeli inavyo karibia tukuwe katika Imani na upendo tuweze kusheherekea.

Sala:
Bwana, kipindi cha Noeli kinavyokaribia kabisa tunakuomba tuweze kukuwa katika Imani na kusheherekea ujio wa Kristo, ambaye ni Bwana milele na milele. Yesu anakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni