Ijumaa. 18 Oktoba. 2024

Tafakari

Jumatano, Septemba 28, 2016

Jumatano, Septemba 28, 2016.
Juma la 26 la Mwaka


Ayu 9: 1-12, 14-16
Zab 87: 10-15
Lk 9: 57-62


GHARAMA YA KUWA MFUASI WA KWELI WA KRISTO!

Tunaishi katika ulimwengu ambao gharama za maisha zinapanda kadiri ya mahitaji yanavyopanda. Na wakati mwingine kadiri gharama inavyopanda ndivyo tunavyo hitaji zaidi. Kuna gharama ya kumfuata Kristo pia! Katika Injili, watu watatu wanakuja kwa Yesu na wanataka kumfuata. Lakini Yesu alivyo ongea kuhusu gharama ya kumfuata hawakuwa tayari kuilipa. Walitaka kuwa na Yesu lakini katika hali yao wenyewe. Hawakuwa tayari kuachia mambo yao, tamaa zao, mipango yao n.k, kwa ajili ya Kristo.

Haishangazi kwamba Yesu alisema njia ya kwenda kwenye uzima wa milele ni nyembamba na ni wachache watakao ipata. Ayubu ni mtu ambaye anajulikana kwetu kama mtumishi mwaminifu wa Mungu. Alikuwa mzuri kwa wengine na alibarikiwa na mengi, alikuwa na familia, afya njema, na kwa wakati, utajiri mwingi. Alikuwa na mitizamo na ndoto za maisha. Lakini yote yalibadilika na Ayubu akapoteza kila kitu.

Somo la kwanza la leo, linamuonesha Ayubu baada ya kuteseka kwa mateso ya kupoteza yote, na pia mtazamo wa Ayubu juu ya Mungu unabadilika vile vile. Mwanzoni alionekana kuwa na uchungu. Lakini mwishoni Ayubu alichagua kujitegemeza kwa Bwana. Kwa kuangalia mfano huu, tunaweza kuona ni kwanini tunaambiwa tutoke katika njia zetu ili Bwana aingie afanye kazi yake. Kufanya yote haya yanahitaji kujikabidhi kweli kwa Mungu, dunia inaweza isikuelewe na hata marafiki wanaweza wasikuelewe na hata kukutenga, kwasababu wakati mwingine inakupasa kufanya kinyume na mtazamo wa dunia inavyodhani. Je, upo tayari kulipa gharama ili uwe mfuasi wa kweli wa Kristo?

Sala: Chukua Ee Bwana, na pokea uhuru wangu wote, kumbukumbu zangu, uelewa wangu, na mapenzi yangu. Vyote jinsi nilivyo na yote niliyonayo umenipa. Nipe tu upendo na neema yako-kwa haya nitakuwa tajiri kabisa na sitatamani kingine zaidi. Amina. (Sala ya Mt. Inyasi wa Loyola)

Maoni


Ingia utoe maoni