Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Oktoba 24, 2018

Jumatano, Oktoba 24, 2018,
Juma la 29 la Mwaka wa Kanisa

Ef 3:2-12;
Is 12:2-6;
Lk 12:39-48


UFUASI: WITO WA KUWA MWAMINIFU, SI KWA AJILI YA MAFANIKIO!
Uaminifu na ukweli ni mambo makuu matakatifu na mazuri kabisa yaliowekwa kama zawadi katika akili ya mwanadamu. Kuwa mwaminifu katika mambo madogo sana ni njia ya kuelewa, kuboresha, na kuelezea nguvu itakiwayo kutenda mambo makubwa. Uaminifu si kutenda mambo sahihi mara moja tu nakuacha, bali kufanya mambo sahihi mara zote na zaidi ya kawaida. Mfano katika Injili unatutaka sisi kuwa tayari, kuwa waaminifu kila wakati, tutende mema na kuwa waaminifu si kwasababu tunaogopa siku ya mwisho bali tutende wema na kuwa waaminifu kwani ndio tabia ya Kimungu.

Je, kadiri ya Yesu nini maana ya uaminifu? kuyashika maneno ya mtu husika, ahadi, na majitoleo, bila kujali unapata ugumu au hatari ya namna gani. Uaminifu ni sifa ya msingi ya Mungu na ndiyo anayoitegemea kutoka kwetu. Bahati nzuri Mungu pia anatoa neema na nguvu ya kutusaidia kubaki waaminifu na anatarajia sisi tuvitumie vema vipaji na neema atukirimiazo sisi. Wale wote wanaojua mwalimu wao anahitaji nini (kama wafuasi wake) lakini wanatenda mambo mabaya atakapo rudi atawaadhibu vibaya sana. Wale wote wasio jua (wasio wafuasi, watu wa nje) bado wataadhibiwa kwa kufanya makosa lakini adhabu yao itakuwa ndogo. Basi tusijifanye kuwa wajinga na kuziacha kazi na majukumu yetu. Imani katika kipimo cha ukamilifu hutufanya sisi kuwa ‘waaminifu’ na wakati tukiwa waaminifu, watu wanapata matumani ‘kujiaminisha kwetu na kwa pamoja tunajiunga na kumwamini Mungu na kuwa mwaminifu kwake. Je, sisi tu waaminifu kwa Mungu na tupo tayari kumtolea yeye hesabu ya uaminifu wetu?

Sala:
Bwana tusaidie sisi tuwe waaminifu daima, kwasababu katika uaminifu tunapata nguvu zetu.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni