Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Oktoba 16, 2018

Jumanne, Oktoba 16, 2018,
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa

Gal 5:1-6
Zab 118:41, 44-45, 47-48
Lk 11:37-41


YESU ANAYASEMA YOTE KWA UWAZI

Mafarisayo walijivuna nakujiona wao wenyewe kuwa wema na wasafi kwa kushika mapokeo na sheria. Waliigawa jamii katika makundi ya walio wema na walio wabaya, wakijiona wenyewe kuwa wema na watu wamataifa mengine kuwa waovu. Kwa njia ya taratibu na sheria zilizo tengenezwa na wanadamu walifunga ufalme wa Mungu kwa watu wa mataifa mengine (waliodhani hawastahili wokovu). Walijifanya kuonekana wasafi na wema kumbe mioyo yao ilikuwa minafiki na miovu. Yesu anaonya juu ya unafiki wao wa kila wakati.
Mungu anaisoma mioyo ya watu. Kama ndani ya mtu ni giza, mwili wote unakuwa giza na mtu hawezi kujidai ni mtu wa Mungu. Yesu anatoa ujumbe mkubwa kabisa kwa wote, hasa kwa viongozi wa dini, wawe watu wa Mungu kweli, wenye tabia za Kimungu, utu na maadili mema. Ni mtu mzuri tu anayeweza kuzaa matunda mema ya roho, ambayo ni , “upendo, furaha, Amani, upole na kujitawala” (Gal 5:22 – 23).

Katika Injili tunamuona Mfarisayo anamualika Yesu kwa chakula. Yesu alifahamu lengo la Mfarisayo kumualika kwa chakula cha pamoja. Walitaka kutafuta kosa ili wamhukumu Yesu. Lakini Yesu anachukua nafasi hii kurekebisha mawazo yao. Yesu alikuwa mtu mwazi. Alienda kwa chakula cha pamoja na akawarekebisha. Sisi nasi tuna nafasi mbali mbali za kuwarekebisha watu wengi tunaokutana nao katika maisha yetu. Je, tupo tayari kusema ukweli kwa ajili ya kuleta marekebisho mema na kutokomeza uovu? Au tunasubiri mpaka mtu akosee ili tufurahi na ndipo tunapoenda kumweleza ukweli? Je, matendo yangu katika dini yangu yananifanya niwe chombo cha Amani na umoja katika jamii ninayoishi?

Sala:
Bwana, tufanye waaminifu na wakweli. Tupe utambuzi wa unafiki wowote mahali popote, lakini usituache tusahau unafiki wetu wenyewe. Tusaidie tuweze kutambua kuwa mabadiliko haya kama mengine yanapaswa yaanzie ndani maana yake ndani ya mioyo yetu na akili zetu.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni