Jumapili, Oktoba 14, 2018
DOMINIKA YA 28 YA MWAKA B WA KANISA
Somo la kwanza,Hek 7:7-11
Hekima ni zaidi ya dhahabu au utajiri wowote. Ukiwa na hekima ya Kimungu una utajiri mkubwa sana. Bora kukosa mali za dunia kuliko kukosa hekima hii ya Kimungu. Mtu akiwa na mali nyingi sana na hata akipata dunia yote akimkosa Mungu, kwakweli ni maskini wa mwisho kabisa.
Wimbo wa katikati
Zab 90:12-13,14-15,16-17
Bwana anatujaza Upendo na furaha. Ndiye anayetushibisha kwa fadhili zake. Kila kilichopo duniani ni fadhili za Bwana, ndiye anayetufanya sisi tufurahi kwasababu ya fadhili hizi. Ili kuzifurahia zaidi ni lazima tuhakikishe tuna uhusiano mwema naye. Ukiwa na wingi wa hizi fadhili zake na ukamsahau kweli ni bahati mbaya kabisa.
Somo la 2
Ebr 4:12-13
Neno la Mungu linaufungua moyo. Anayelisikiliza neno la Mungu kwa unyofu hatakosa lolote la kumsaidia katika maisha yake. Kiburi cha mali chaweza kutufanya tukatae na kutoruhusu hili neno likuwe na kuleta matunda.
Injili
Mark 10:17-30
Kijana mmoja anamuuliza Yesu, afanye nini ili apate kuurithi uzima wa milele? Tunaona hatari ya kuridhika kwa kupata faraja katika mali za dunia inapoweza kutufanya tukapata ugumu wa kumfuata Mungu.
HATARI YA MALI KUCHUKUA NAFASI YA MUNGU
Katika jumapili ya leo tunaendelea kusoma Injili ya Marko tena tunaendelea pale tulipo achia Jumapili iliyopita. Jumapili iliyopita, tuliona jinsi gani Yesu alivyo jaribiwa na Mafarisayo kuhusu talaka. Tutambua hapa Yesu alikuwa njiani akielekea Yesusalemu.
Katika Injili ya leo, kijana ambaye hakutajwa jina lake anamfuata Yesu na anamuuliza atafanyeje ili aweze kuurithi Ufalme wa Mbinguni? Yesu anamjibu kwamba ni lazima kuzishika Amri za Mungu alizowapa kupitia Musa. Kijana huyu anakiri kwamba amekuwa akizishika tangu utoto wake. Yesu anamwambia amekasoro kitu kimoja, anapaswa kuwapa mali zake maskini na ndipo amfuate. Huyu kijana tunaambiwa kwamba aliondoka kwa huzuni kubwa. Marko anatueleza kabisa ni kwanini? Ni kwasababu alikuwa na mali nyingi. Ni ajabu kidogo kuwa na mali nyingi tungetegemea kwamba ingekuwa rahisi kwake kwamba angekimbia kwa furaha na kugawa badala yake mwenye mali nyingi anagoma na kuona uchungu. Hili linawatokea wengi hadi leo hii. Walio na mali nyingi huteseka na kujishughulisha mnoo na kukosa muda wa Mungu kuliko wale wenye mali kidogo.
Imani kuhusu ufufuko na pia uzima wa milele ndiyo kwanza ilikuwa ikifundishwa kwa baadhi ya wachache waliokuwa wakiamini. Mafarisayo waliwafundisha watu kuhusu kufufuka na kupata uzima wa milele. Masadukayo hawakukubali ufufuko wa wafu. Lakini Yesu alivyokuja alifundisha kuhusu ufufuko wa wafu na pia kutakuwa na hukumu ya mwisho kwa kila mmoja na maisha ya ufalme wa Mungu ya milele. Hili ndilo lililomfanya huyu kijana kutafakari na mwishowe kuishia kumuuliza Yesu swali kuhusu namna ya kutenda ili aweze kuingia katika ufalme huo. Masharti yakaonekana kuwa magumu kwake.
Kumfuata Yesu kwanza ni lazima kwanza kutoshikamana na malimwengu. Hili katika historia watakatifu wengi wamelielewa kwa nmna yao. walijikita kwenye injili na kuamua kujikatalia matamu ya dunia hata wengine walienda kuishi maisha ya kujitenga na kupata muda mwingi wa kusali. Kwa namna nyingine pia ni kujikatalia mambo yote ambayo yanatufanya tushindwe kumfuata Yesu. Hivyo kumfuata Yesu tunapaswa tumfuate na tujue kwamba ulinzi wa kweli upo kwake na si katika mali tulionayo. Tusitafute ulinzi katika mali tulizonazo. Ulinzi wa kweli na Amani ya kweli ipo kwa Yesu.
Wito huu wa Yesu kwenye Injili ni mwaliko kwa kila mfuasi wa Yesu. Wito kwa wale wote wanaopenda kumfuata Yesu kwamba wawe tayari kumpenda yeye zaidi kuliko chochote. Yesu alifurahi baada ya yule kijana kuonesha kwamba anashika amri vizuri. Laikini pia Yesu alihuzunika sana baada ya kuona yule kijana akishindwa kuwa tayari kuachia mali ili aweze kumfuata. Sisi nasi Yesu anahuzunika kweli anavyoona sisi tumeshikamana na vitu na mali nyingi tukashindwa kumfuata kwa moyo wote. Tusimhuzunishe Yesu kwa kupenda mali mnoo kupita kiasi. Mali zako zisikufanye uone muda wa kukaa na Yesu kama mzigo mkubwa sana.
Pamoja na kwamba Yesu ameonesha ni kwa jinsi gani ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia mbinguni. Bado Yesu anawaonesha wafuasi wake hakuna kitu kisicho wezekana kwa Mungu. Wongofu unawezekana kwa kuweka matumaini yetu yote kwa Mungu.
Petro kwa kutaka kuchokoza zaidi, anamuuliza Yesu kwamba mitume nao wameacha vyote wakamfuata watapata nini zaidi. Yesu anakiri kwamba wale walioacha vyote kwa ajili ya Injili watapata thawabu kubwa. Na thawabu hiyo inaanza sasa, ataifurahia hapa duniani na baadaye hata huko Mbinguni. Sisi tujitahidi ndugu zangu tusibaki nyuma kwa kusongwa mnoo na malimwengu tushindwe kupata furaha hii ya Injili. Kweli kwasasa watu wanasujudu mali mnoo kupita kiasi, hata utu wa watu umepunguzwa na utaheshimiwa tuu kama wewe una mali.
Wakati mwingine mali imetufanya tuwatenge baadhi ya watu kwani tunaona kana kwamba hawana thamani ya kukaa nasi. Kukaa nasi pengine lazima awe na nyumba zuri au gari tena la bei Fulani. Mali inakishawishi kikubwa sana kwani, mali yaweza kukufanya uwe na maringo na majivuno makubwa kiasi cha kukataa hata dhambi zako mwenyewe. Kwasababu ya mali ulizon azo waweza kushindwa kuona hata makosa yako kwani waweza kujifariji kwamba mtu mwenye mali kama mimi siwezi kuwa na dhambi. Hili limewadumbukiza wengi kwenye shimo. Tujitahidi kuwa na Mungu katika maisha yetu. Kuwa na Mungu ni kuwa na vyote kwasababu vyote ni vya Mungu.
Maoni
Ingia utoe maoni