Ijumaa, Septemba 07, 2018
Ijumaa, Septemba 7, 2018,
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa
1Kor 4: 1-5;
Zab 36: 3-6, 27-28, 39-40;
Lk 5: 33-39
HAKUNA KIRAKA; HAKUNA KUCHANGANYA!
Leo Yesu anatumia mfano wa viriba vinavyotumika kuhifadhia divai ili atufundishe lengo letu la kuja Ulimwenguni. Kama ilivyo vigumu kwa divai mpya kukaa kwenye viriba vikukuu, mafundisho ya Yesu hayawezi kuendana na namna yetu ya maisha ya dhambi na jinsi ya kufikiri kama zamani. Kumkubali Yesu na mafundisho yake ina maana kwamba kuanza maisha mapya. Hakuna kuchanganya maisha ya zamani na maisha mapya, lazima kuacha maisha ya dhambi na kuanza maisha mapya. Unavyoitwa na Yesu kuna labda uitike “NDIYO” au “HAPANA”. Ndiyo ikimanisha kwamba unafanywa kiumbe kipya kabisa na kuanza maisha mapya au Hapana ukimanisha umekataa na umeamua kuishi katika maisha ya zamani ya dhambi na kubaki katika hali mbaya. Tuombe neema ya Roho Mtakatifu ili sisi tuliosema ndio tusichanganye tena maisha haya mapya na maisha ya dhambi, maisha ya kale.
Tukienenda katika “NDIYO” yetu ndani ya maisha mapya ndani ya Kristo, kama Mt. Paulo anavyosema katika somo la kwanza, watu watatuhesabu kuwa watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri ya Mungu. Na furaha yetu haitakuwa kwasababu watu wametuhesabu kuwa watumishi wa Kristo bali ni kwasababu Mungu atatuhesabu kuwa mawakili wake hapa duniani. Kwani hata hivyo Mungu akituhesabia haki ninani tena awezaye kutuhukumu? Hakuna yeyote wala nafsi zetu wala mwanadamu yeyote. Kwakuwa furaha yetu itakuwa katika Bwana daima.
Sala:
Bwana Yesu, nisaidiye kubadili maisha yangu kwa mwanga wa Neno lako.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni