Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Septemba 02, 2018

Jumapili, Septemba 2, 2018.
Dominika ya 22 ya Mwaka B wa Kanisa

Kumb 4: 1-2, 6-8;
Zab 14: 1-5;
Yak 1: 17-18, 21-22, 27;
Mk 7: 1-8, 14-15, 21-23.


MOYO WA KUABUDU
Nilichukua simu na kumpigia rafiki yangu. Nilitaka kupata ushauri kuhusu mambo yangu binafsi. Gafla kabla ya kubeba simu nikasikia simu ikiita na baada ya kupokea nikakuta ni ujumbe wa sauti unaosema, “mimi sipo nimetoka nimeenda mbali nitarudi jioni nitakutafuta”. Sauti ni ya rafiki lakini yeye mwenyewe hayupo. Kumbe ni simu tuu nashika na sauti ilirekodiwa muda mrefu. Hivi ndivyo wakati mwingine tunavyo enda kwa Mungu. Wakati mwinngine sauti yetu ipo inamsifu Mungu lakini mioyo yetu kwakweli haipo pale. Nikama sauti iliyorekodiwa.

Leo tunakumbushwa kuhusu Mungu kuja kwetu mara nyingi lakini kwa uhalisia Mungu hatukuti sisi, tumekuwa tu kama simu na mioyo yetu haipo pale. Yesu aliwaambia Mafarisayo “hawa watu wananiheshimu kwa midomo yao tuu lakini mioyo yao ipo mbali’. Mara nyingi sisi kama Mafarisayo tunaweza kuwa kanisani tukawa tunatoa sauti na kusifu lakini mioyo yetu ipo mbali mno.

Katika somo la kwanza Musa anawakumbusha wana Waisraeli mambo yote ambayo Mungu ameyatenda na anawaalika wawe waaminifu. Kwa njia ya tukio la safari kutoka Misri na kwa njia ya Agano la Sinai Mungu alionesha upendo wake kwa Israeli na aliwataka waisraeli wajibu upendo huo kwa kuonesha upendo kwa Mungu kwa kushika amri zake.

Katika somo la pili Yakobo anasema mambo yale yale kama Musa alivyosema, lakini kwa maneno mengine. Anawaambia wasomaji wake kwamba wasiwe wasikilizaji tu waneno la Mungu lakini pia walitende. Na kutenda huku kunapaswa kuonekane kwa kuwajali maskini na wale wanao onekana kutengwa na jamii.

Injili imebeba sehemu mbili: anawaasa Mafarisayo kushika mapokeo ya wazee na kuyafanya kana kwamba ni amri za Mungu na kutangaza mambo ya mila za Wayahudi ili kutimiza haja zao binafsi. Yesu anawalaumu kwa kufanya hali ya kumwabudu Mungu kuwa kama sehemu ya kufanya kwa nje nje tuu ili kutazamwa na watu. Matendo hayo yanapaswa kupata mizizi katika moyo.

Yesu anatualika sisi tuwatazame wale ambao wanasisitiza sheria zinazokosa mapendo. Na wale ambao wanatazama sana mambo ya kibinadamu na kuyajali sana na badala yake kuacha kushika mambo ya Mungu. Na mtazamo huu nikutaka sisi tuache kusifu kwa midomo na badala yake tutende kutoka ndani ya moyo wetu. Yesu anawaalika wasikilizaji wake kwamba yeye hataki mambo ya nje nje tuu bali moyo wa kweli na wenye kutenda kweli. Wanaitwa kutenda mambo makuu ambayo yanapaswa kuwa na mizizi ndani ya mioyo yao na sio kwa midomo pekee.

Mt. Teresa wa Avilla anasema kwamba”ndani Mwako yupo Mungu. Ingia ndani na mtazame yeye ndani ya moyo wako”. Je, ni nini kilichopo ndani ya moyo wako? Unapopata muda wa kukaa pekee yako na kujitazama ndani unaona nini? Je, moyo haujajazwa na uongo na udanganyifu wa kila aina? Haya hayatakujenga badala yake yatakubomoa. Yesu anaendelea kutuita. Yeye aliwaita watu wakipindi hicho miaka 2000 iliyopita na sasa anaendelea kutuita sisi ili tuweze kuwa na mioyo isiyo na hatia mbele ya Mungu. Na ulimwengu huu patakuwa ni sehemu njema ya kutangaza ufalme wa Mungu.

Sala:
Bwana, naomba uje ndani ya moyo wangu. Ninakuomba ufanye moyo wangu uwe katika moto wako ili uweze kuangaza kwa wote ili waweze kuona. Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni