Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Septemba 01, 2018

Jumamosi, septemba 1, 2019,
Juma la 21 la mwaka wa Kanisa

1Kor 1:26-31;
Zab 32:12-13, 18-21;
Mt. 25:14-30


WEMA WA MUNGU!
Mungu ni muumba wetu, anayetulinda na kututegemeza. Anatupa maisha kila wakati. Upendo wake kwetu usio na mwisho hauwezi kuondoshwa na yeyote. Anatimiza mipango yake kwa jinsi yake na anawatumia watu wake na vitu kutimiza hayo. Mt. Paulo anatukumbusha kwamba wito wetu ni zawadi safi, tuliopewa sio kwa wakubwa wa ulimwengu bali walio wadogo. Wema wetu, utakatifu wetu na ukombozi wetu unatoka kwake yeye. Tunapaswa tuwe wazi kwa wito huu na kuitikia vizuri.

Tunaona nini leo katika Injili: kuna bwana mmoja ambaye ni tajiri sana na anapenda na kutarajia mazuri ya wafanyakazi wake na anawaamini, anawakabidhi sio katika kiwango kidogo, bali katika kiwango cha talanta ya chini (talanta ilikuwa ni hata zaidi ya mishahara ya miaka kumi na tano ya mshahara wa mfanyakazi). Mungu ametuumba sisi kwasababu ya upendo na anatuongoza kadiri ya upendo wake. Anatupa neema na nguvu tele. Wote hawapewi Baraka ile ile na vipaji vile vile. Hata yule tunayedhani kapewa kidogo, amepewa vingi sana. Ni kweli kwamba wote hatujapewa sawa. Akili ya kibinadamu haina majibu kuhusu hili. Lakini tutahukumiwa kama hatutatumia vipaji tulivyopewa.

Tutambue tumepewa vipaji tofauti na kwa vipaji hivyo tutumie ili pale panapo onekana kupungua kwa mwingine, basi yule aliyepewa zaidi aweze kujazia pengo hilo. Kwa njia hiyo sisi wote tutasonga mbele kama mwili mmoja wa Kristo ulio na viungo tofauti vyenye kushirkiana kwa upendo. Hakuna aliyebora zaidi kuliko mwingine mbele ya Mungu kama wote tutazishika amri zake na kutembea katika upendo wake.

Kikwazo kikubwa kinacho tufanya tushindwe kushirikishana vipaji vyetu alivyotupa Mungu ni wivu mbaya. Watu hawapo tayari kukuona umefaulu jambo fulani kwasababu ya kipaji chako, wengine waweza kufanya jambo lakini kwasababu ni yeye, wengine wanasema haiwezekani huyu afanye jambo hili, (ni sawa na kusema yawezekana jambo jema litoke nazareti?). Huenda wengi wetu tumeviua vipaji vya wenzetu kwasababu ya kulinda ukubwa wetu na kutaka kuonekana sisi tu, pengine tumeshindwa kumpokea kiongozi mwenzetu aliyechaguliwa katika jumuiya au jamii yetu kwasababu tunadhani hawezi kutupa chochote kipya. Ndugu zangu kila tufanyalo tujaribu kujiweka katika miguu ya Kristo, kwamba ingekuwa Kristo angefanya hivi? Je Kristo hakutenda yote kwa upendo mkubwa tena kwakuwahurumia wadhambi walioonekana kama hawafai katika jamii? Tuombee neema ya Mungu tuwe na moyo wakuwapenda wenzetu na kuwasaidia kujenga na kuimarisha vipaji na karama zao walizopewa na Mungu, ili wote kwa pamoja na kwa njia yetu Mungu arudishiwe sifa na utukufu.

Sala:
Bwana, naomba unipe hekima niweze kutumia zawadi na vipaji ulivyonipa vizuri.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni