Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Agosti 12, 2018

Jumapili 12, 8, 2018.
Dominika ya 19 ya Mwaka wa Kanisa

1 Fal 19: 4-8;
Zab 34: 2-9 (R) 9;
Ef 4: 30 – 5: 2;
Yn 6: 41-51.


EKARISTI CHAKULA CHA WASAFIRI
Kulikuwa na Binti Mmoja alikuwa akiitwa Mary alikuwa akiishi na ndugu yake mwingine anayeitwa Cathe. Siku moja Mary alipatwa na ugonjwa mkali akakaimbizwa hospitalini. Hali yake ilikuwa mbaya sana na alikuwa akiongea kwa taabu sana. Mary akiwa hopitali alikuwa karibu na dirisha na katika hali yake ya ugonjwa, Cathe alivyo ingia hospitalini alimkuta Mary akitazama njee huku akihesabu kinyume ….kumi…tisa…nane..saba. sasa Cathe alishangazwa kwanini anafanya hivyo huku akitazama nje, Cathe aliamua kutazama nje aone kuna nini? Akatazama lakini hakukuwa na kitu chochote kinachovutia. Lakini kulikuwa na mti mkubwa ambao ulikuwa umepuputua majani yake lakini yalikuwa yamebaki machache. Cathe akamuuliza Mary kwanini unahesabu hivyo Mary akamwambia ninahesabu majani yanayo anguka na hivyo jani la mwisho litakavyo anguka na mimi itakuwa ndiyo mwisho wa maisha yangu. Cathe baada ya kusikia hivyo alivuta kateni la dirisha na kulifunga dirisha. Mary alivyo amka tena kesho yake, aliomba kateni liondolewe atazame njee, baada ya kutazama akakuta majani ya mti yamepungua tena sana. Akasema sasa najiandaa kuondoka huenda kesho jani la mwisho litaondoka. Alivyo amka akakuta jani moja tuu limebaki. Na hapo akasema sasa nalisubiri lidondoke na hapo itakuwa ndio mwisho wa maisha yangu. Cathe akavuta kateni akafunga dirisha. Cathe akatoka njee akaenda kumtafuta kijana mmoja anayeitwa Benson. Akamuomba aende apande kwenye mti na kushikilia lile jani kwa gundi kali. Yule kijana akajitahidi akafanya hivyo. Kesho yake Mary akaomba kateni lifunguliwe aweze kuona nje kama jani lipo, na wakati huu kwasababu anajua kwa hakika jani lilibaki moja ni wazi kwamba litakuwa limeanguka. Baada ya kufungua kateni tazama jani bado lipo. Akapata nguvu akafurahii, baada ya muda afya ikaanza kurudi baada ya kuona kwamba kumbe bado Mungu ananipenda, akawa anashangaa lile jani bado lipo kila siku akaendelea kupata nguvu nahatimaye akatoka hospitali na kuelekea nyumbani na akapata afya na maisha yakaendelea. Hali ya Mary ya kukata tamaa inafanan nay a nabii Elia katika somo la kwanza.

Katika somo la kwanza tunakutana na mtu wa Mungu, anayejulikana katika Agano la Kale kama nabii mkuu, Elia. Lakini tunakutana naye akiwa katika hali ya mahangaiko. Jezebeli alikuwa akimwinda na kutaka kumua. Sasa afanye nini? Ilibidi akimbilie jangwani na huko anapatwa na gadhabu na anafikia mahali anajiona kwamba sasa anapaswa kufa kwasababu kila alichofanya kimeisha. Hivyo anamuomba Mungu achukue maisha yake. Lakini badala ya kufanya hivyo Mungu anamtuma Malaika amletee chakula na maji. Baada ya kupewa chakula hiki Elia anapata nguvu na kupanda kuelekea mlimani kwa Bwana kukutana na Mungu. Katika mlima Horebu alikutana na Mungu na hivyo akapata nguvu mpya ya kuendelea kumtumikia Mungu. Wakati dhoruba ikija kwetu na mahangaiko mengi sisi tunakata tamaa na kuwa kama Elia. Tunalia na kuhuzunika na wakati mwingine kumwambia Mungu achukue maisha yetu. Tunachofanya ni kwamba tunafunga milango yetu kwa Mungu na kutokumrushusu aingie katika maisha yetu atusaidie. Ili kuwa na nafasi ya Mungu yakuingia katika maisha yetu, tunapaswa kuwa watu wanaokutana na Mungu katika sala.

Katika somo la pili kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso, Paulo anasema, sisi wote tumetiwa alama ya Roho Mtakatifu. Hivyo tunapaswa kuondoa utengano wowote ule, uwe uchungu, hasira mbaya nk., nakuwa na fadhila kama ukarimu, huruma na msamaha.
Na katika Injili Yesu anatoa fundisho kubwa sana kuhusu Ekaristi Takatifu, mwili wake mwenyewe, mkate wa uzima. Anasema kwamba mimi ni mkate ulioshuka kutoka Mbinguni; atakaye kula chakula hiki ataishi milele na mkate nitakao toa ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu”.

Kila jumapili au kila siku kama tunaenda kanisani, tuna bahati ya kupokea mkate huu wa uzima ambao ni mwili wa Kristo, Umungu wa Masiha. Mfalme wa Wafalme, Mkombozi wa ulimwengu, aliyekuwepo Daima na Mungu wa Utukufu! Lakini je, sisi tunafanya nini? Pengine tunakuja kanisani tukiwa kama hatutaki, tukiwa na mawazo makuuu ya yale tutakayo yafanya baadae. Na huu ndio ukweli wenye huzuni ndani yake. “Kama tungefahamu ukuu wa zawadi ya Misa Takatifu tungekufa ndani yetu kwa mapendo makuu” alisema Mt. Yohane Maria Vianey. Je unafahamu ukuu wa misa? Badilika leo na anza maisha mpya kwa kuyapa mambo ya Mungu nafasi ya kwanza. Hili linalo kuchosha ndilo la muhimu siku ya mwisho kuliko unayo yahangaikia.

Tafakari leo kama moyo wako umeungana na Ekaristi Takatifu. Je, wakati unafikiria kwenda kwenye misa unajisikia furaha na ile hali ya furaha kana kwamba unaenda kwenye sherehe Fulani? Au unalitazama hili kana kwamba ni jukumu tu la kawaida la kutimiza na kuondoka? Tujitahidi ili Mungu aendelee kutubariki.

Sala:
Bwana, nisaidie mimi niweze kukuona wewe katika Misa Takatifu. Nisaidie mimi niweze kukutamani wewe katika Ekaristi Takatifu. Ninakuomba nisikose Imani thabiti na kujitoa. Ninakuomba nijazwe kwa mapendo makuu katika zawadi hii Takatifu. Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni