Jumatatu, Julai 30, 2018
Jumatatu, Julai 30, 2018.
Juma la 17 la Mwaka
Yer 13: 1-11;
Kumb 32: 18-21;
Mt 13: 31-35.
MKUBWA MACHONI MWA MUNGU
Yesu akiongea kuhusu Ufalme wa Mbinguni alisema, “Ufalme wa Mungu upo kati yenu” (Lk17: 21). Tunaitwa leo kuufanyia kazi ufalme huu wa Mungu. Tunaweza kuwa na shida ni wapi pa kuanzia. Yesu anatuambia kwamba hata punje ndogo kabisa ya haradali inaweza kukuwa na kuwa mti mkubwa kuliko miti yote ya mboga na kuzaa matunda mengi. Katika hali hiyo hiyo tendo dogo kabisa linaweza kukuwa na kuchangia katika ukuwaji wa ufalme wa Mungu. Kwasababu Ufalme wa Mungu upo kati yetu tunaweza kuanza kuufanyia kazi kwa kuanzia ndani yetu. Kwa kuepukana na mawazo yetu mabaya, njia mbaya na kutembea katika haki hii inaweza kuwa njia ya kuanzia. Kwa muda wake jambo hili linaweza kukuwa na kuwa mti mkubwa sana ambapo ndege wa angani wanaweza kuja kupata pumziko. Ukarimu mdogo kabisa wa familia yangu unaweza kunyanyua juu kabisa familya yangu nakuwa shuhuda mkubwa wa ufalme wa Mungu. Na hivyo ufalme wa Mungu huweza kukuwa na kusambaa.
Mara nyingi tunashawishika kutaka kuona maisha yetu sio muhimu kama ya wengine. Tunaweza kuwatazama wengine ambao wapo na “nguvu” na umaarufu. Natamani kama ningekuwa na fedha zao au kama ningekuwa maarufu kama yeye, mara nyingi tunaanguka katika kishawishi cha “kama ningekuwa mtu fulani”. Mbegu dogo sana inakuwa kubwa kabisa. Na hili linatufanya tuulize swali je, tunajiona wadogo sana? Ni kawaida wakati mwingine kujisikia kana kwamba wewe sio wa muhimu na kufikiria kwamba napaswa kuwa zaidi. Lakini ukweli ni kwamba hii ni hali ya kiulimwengu na kufananishwa na ndoto za mchana. Ukweli ni kwamba kila mmoja wetu anauwezo wakuleta mabadiliko katika ulimwengu. Mbele ya uso wa Mungu tumejazwa mambo mengi sana zaidi ya yale ambayo tunayawaza.
Nini maana ya kubadilishwa na Yesu na kuwa “mti mkubwa” kama punje ya haradali inayomea? Ina maana kwamba tumeitwa na Mungu kutimiza mapenzi yake vizuri na kwa ukamilifu. Ni mpango huu ambao utazaa matunda makubwa na ya kudumu.tunaweza tusipate umaarufu hapa duniani. Lakini ukweli ni kwamba kinacho hitajika ni kwa jinsi gani ulivyo mtakatifu na nikwa jinsi gani umetimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yako.
Mt. Teresa amesema mara nyingi, “tumeitwa kuwa waaminifu na sio maarufu”. Ni uaminifu huu kwa Yesu unaohitajika.
Sala:
Bwana, ninatambua kwamba bila wewe mimi si kitu. Bila wewe maisha yangu hayana kitu. Nisaidie mimi niweze kufuata mapenzi yako matukufu na mpango wako katika maisha yangu ili niweze kupokea lile taji ambalo umeniandalia mimi. Yesu nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni