Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Julai 23, 2018

Jumatatu, Julai 23, 2018.
Juma la 16 la Mwaka

Mik 6: 1-4, 6-8
Zab 49: 5-6, 8-9, 16-17, 21, 23;
Mt 12: 38-42


MKUBWA KULIKO YONA

Kuna watu kati yetu ambao daima hawana furaha, haijalishi umewatendea nini, daima hawana raha na wanalalamika daima. Licha ya makubwa ambayo Bwana amewatendea bado hawaridhiki. Daima Wayahudi walitaka ishara ili kuhakiki ukweli wa unabii. Hawakumtambua Yesu na hivyo wanahitaji ishara zaidi ili waweze kumkubali Yesu. Lakini ukweli ni kwamba hata Yesu angefanya ishara nyingine zaidi bado wasingebadilika. Hata alivyo mponya yule mgonjwa aliyekuwa bubu na kipofu (Mt 12:22), walimlaumu kwa kufanya ishara hizi kwa kutumia mkuu wa pepo.

Yona alikuwa ishara. Alikaa muda wa siku tatu katika tumbo la nyangumi. Ni wazi kwamba walidhani ameshakufa. Lakini nyangumi huyu alitumika kama chombo cha kumfanya Yona atubu na kwenda kupeleka ujumbe Ninawi ili watubu. Walitubu kweli na kubadili maisha yao. Giza ndani ya tumbo la nyangumi, mwishoni limekuwa ni baraka na ishara ya daima. Ishara ya Yona ilikuwa ni ishara ya kifo cha Yesu, mwili wake kukaa siku tatu katika ardhi na baadae kufufuka. Hii ndio ishara ambayo Yesu anatoa na ambayo ataendelea kutoa. Ni ishara ya matumaini makubwa tukiitazama vizuri.

Sisi mara nyingi twaweza kuanguka katika kishawishi hicho hicho. Mara nyingi tunahitaji ishara licha ya ishara mbali mbali ambazo Yesu anazotupatia. Mara nyingi tunataka ishara kutoka kwa Mungu. Tunamtaka yeye aongee kwa sauti na kwa ufasaha. Yesu Kristo yupo nasi daima, akituponya sisi na magonjwa yetu. Yesu yupo ndani ya jirani tunayekutana naye. Ishra kubwa kabisa ni Mungu kuwa Mwanadamu na neno kuwa mwili/chakula kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.

Yesu anatukumbusha kwamba tunapaswa kuamini yale yote anayotuambia hata kama tunajisikia tupo kwenye giza na taabu katika tumbo la samaki au kaburini na matumaini yamepotea. Mungu yupo katika kila kitu. Mungu yupo katika kila kitu na yupo kati yetu hata pale tunapohisi yupo kimya. Anaongea na wewe muda wote. Jifunze kutambua sauti yake.

Sala:
Bwana nisaidie mimi nikuamini wewe hata pale ambapo sioni ishara na miujiza kutoka mbinguni. Nisaidie mimi nikuamini wewe hata pale ninapokuwa na wasi wasi na mashaka na udhaifu wangu katika maisha. Ninaomba unipe Imani thabiti niweze kujibu wito wako katika maisha yangu. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni