Jumatatu, Julai 16, 2018
Jumatatu, Julai 16, 2018,
Juma la 15 la Mwaka
SOMO 1
Isa. 1:10 – 17
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 50: 8 – 9, 16 – 17, 21, 23
Mt 10: 34 - 11: 1.
MFUASI WA KRISTO!
Injili haina lele mama, hakuna cha nusu njia, wala njia fupi katika kumfuata Yesu. Injili yake inatualika tuwe na msimamo mmoja tu. Kifungu cha Injili ya leo kimegawanyika katika sehemu kuu mbili, zote zikiwa na mitazamo mbalimbali juu ya utume.
Sehemu ya kwanza inaonesha masharti ya Yesu kwa yeyote yule anayetaka kumfuata. Yesu anahitaji mtu ajikane kwa hali ya juu kabisa, na kama haitoshi, anamalizia masharti hayo akirudia mara tatu maneno, “hanistahili”. Yeyote atakaye kumfuata Yesu anapaswa ajikane mwenyewe kutoka mambo yote ayapendayo na mvuto wa upendo wa asili kama vile, kuwapenda zaidi wazazi na watoto. Yesu haipingi amri ya kuwapenda na kuwaheshimu baba na mama, bali anaweka wazi kuwa hawapokei watu ambao wanajitoa kwake nusu nusu na kwa muda tu. Wafuasi wanapaswa, si tu kuwa tayari kupoteza chochote, bali kupoteza hata uhai wenyewe. Yesu anahitaji mtu awe jasiri kuacha vyote ikiwemo vitu na vitegemewa vyote kwa ajili ya, apendo. Kinachohitajika ni msimamo mmoja na kumpokea na kumkubali kwa moyo mmoja.
Sehemu ya pili ya Injili hii inahusu ahadi yake kuu – zawadi yake na utimilifu wake. “Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.”
Sala:
Ee Yesu nisaidie niweze kukufuata kwa moyo wote.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni