Jumatano. 22 Mei. 2024

Tafakari

Jumapili, Juni 26, 2016

Jumapili, Juni 26, 2016
Dominika ya 13 ya Mwaka C wa Kanisa

1 Fal 19: 16b, 19-21;
Zab 15: 1-2, 5, 7-11;
Gal 5: 1, 13-18;
Lk 9: 51-62.


UHURU NDANI YA KRISTO!

Kujitoa na uhuru vinaonekana kuwa vitu viwili visivyoendana kwa wengi. Lakini masomo ya leo yanatutaka tujitoe bila kujibakiza na kuishi ndani ya uhuru kamili. Liturjia ya leo inazungumzia nini maana halisi ya kuwa mfuasi wa Yesu.
Somo la leo linafungua kwa kuongelea jambo muhimu katika maisha ya Yesu. “wakati muda wake ulipokaribia wakuchukuliwa kwenda Mbinguni Yesu alienda Yerusalemu”. Katika injili ya Luka Yerusalemu ni kiini kikubwa katika maisha ya Yesu. Ni sehemu ambayo kazi ya ukombozi ya Yesu ilijifunua. Ni sehemu ambayo mitume wa Yesu watatengeneza jumuiya mpya ambayo baadae wataanzia utume wao pale na kueneza kwenda pande nyingine. Yesu anaukazia macho mji wa Yerusalemu kwasababu ni sehemu ambayo atatimiliza yote yalioandikwa juu yake na kutimiza kazi yake pale. Moja kwa moja anatoa changamoto ya kujitoa kwetu kwaajili ya utume wake na kuwa tayari kupokea yote yatakoyotokana na kazi hiyo.

Wakati Yesu anaeleza nia yake ya kwenda Yerusalemu watu wanaeleza hamu yao yakwenda naye. Kama ilivyo kwetu sisi, hawakuelewa kabisa ni nini maana ya “kwenda Yerusalemu”, maana halisi ya Yesu na wale aliokuwa nao.

Wakati mmoja na kwa kujiamini mmoja alimuambia Yesu, “nitakufuata kokote utakapo kwenda”. Alikuwa na hamu kumbwa yakumfuata lakini huenda hakujua ukweli utakao mpata kwa kumfuata. Yesu anamrudisha nyuma. Hata mbweha na wanyama wakali wanasehemu ya kuishi lakini mwana wa adamu hana mahali pakulaza kichwa chake, Yesu alimwambia. Kitu kimoja muhimu katika ufuasi anachopaswa kutambua mfuasi, ni kwamba lazima awe tayari kuacha watu, kutofungamana na vitu vya nje. Je nipo tayari? Au ni lazima kujihakikishia usalama wangu wa vitu kwanza na kuvibeba ndiyo nimfuate?

Mtu mwingine wa pili pia alitaka kumfuata Yesu. Alitoa sababu ambayo tunaona ni kubwa kweli, alisema “nikamzike Baba yangu kwanza”. Jibu la Yesu linaonekana kuwa kama sio zuri sana na laukali “waache wafu wazike wafu wao, kazi yako ni kwenda kutangaza ufalme wa Mungu”. Ni kwamba Yesu haseme tusiwapende na kuwahesimu ndugu wa familia zetu. Bali anataka kutuambia, je, nia yangu ya kwanza kabisa nimeiweka kwa nani? Anataka kutuambia kwamba kama tunataka kuwa wafuasi wake hatuwezi kwanza kujitengezenezea mambo yetu alafu ndio tumfuate. Tumfuate yeye kwanza kwa uaminifu na mengine yatakuja kwaziada. Je ni mara ngapi kati yetu tunapanga kwanza mambo yetu alafu ndio tunaanza kuuliza hivi nitakuwaje Mkristo mwema? Wakati inapaswa kuwa kinyume chake?

Mtu wa tatu alisema anataka kumfuata Yesu lakini anataka akaage familia yake kwanza na marafiki, lakini kuwa mfuasi halisi wa Yesu hamna kusitasita. Kuitika wito ni sasa, leo na jibu lazima liwe sasa, leo.

Tunaona kuitwa kwa Elisha katika somo la kwanza, mambo kama hayo yanajitokeza katika kuitwa kwa Elisha ambaye naye alikuwa apokee kazi ya Elia nabii. Elisha alitaka kwanza akawaage wazazi wake. “Nenda, Nenda” alisema Elia. Lakini baadaye Elisha akafikiri vyema juu ya hilo. Akachukuwa ngombe wake akawachinja. Akachukuwa ile miti akawasha moto na kuchoma zile nyama akawapa watu wote. Hii ilikuwa namna yake yakuishi. Akiwa hana kitu sasa anamfuata Elia. Katika hili haimaanishi kuchukulia mambo yetu moja kwa moja kama ilivyoandikwa kwa somo ila vitu tulivyo navyo tuvitumie ili tuweze kufika kwa Yesu, visiwe sababu ya kutuzuia kumfuata Yesu vizuri. Mali, akili yetu, zisituzuie kumfuata Yesu. Tusipo angalia vizuri vitu kama hivyo vyaweza kutufanya tuchechemee tushindwe kumfuata Yesu vizuri. Muda uliomwingi tunaishi maisha nusu nusu au tunaishi maisha ya wengine tunaacha maisha yetu binafsi. Na ndio maana Paulo leo kutoka kitabu cha Wagalatia anasisitiza sana kuhusu uhuru. “wakati Yesu alipotufanya huru alipenda sisi tuwe huru kweli”. Baadhi ya wakristo wa Galatia walikuwa ni Wayahudi na watu wengine waliwahimiza warudi katika hali yao ya zamani ya kushika sheria ya Musa. Watu wanapenda kurudi katika maisha yao ya zamani ya dhambi, hatutaki kuwa huru.

Kuwa huru kwa Paulo, sio kikwazo cha kupata rehema. Kuwa huru sio kukwepa ukweli wa maisha bali kuishi ndani ya maisha yenyewe na kukumbana na changamoto zake. Kuwa huru kabisa maana yake ni kuchukuwa majukumu yako binafsi na kuyatekeleza vyema sio kuweka malalamiko kwa wengine kwasababu ya magumu yako. Sio kujiwekea usalama kwa fedha, au kuwa maskini, cheo, mafanikio, au mali na mambo kama hayo. Watu wenye uhuru wa kweli wanafanya kile kile anachosema kwasababu wanapenda ulimwengu wenye ukweli, wanajali, kushirikisha, wana Amani na usalama wa kweli wa moyo.
Tunaona uhuru wa namna hii kwa watu kama Yesu, Elisha na Paulo. Na zaidi kabisa tunaona haya kwa mfuasi wa Kristo, Mtakatifu Fransisko wa Assis ambaye alipenda kuishi kama ndege wa angani wanavyoishi bila kufungamana na mali na mambo ya ulimwengu. Huyu aliitika wito wa Yesu bila kuweka masharti, kwa maisha yake yanaonesha kuwa mfuasi wa Yesu katika safari ya Yerusalemu. Je sisi nasi tupo tayari kufuatana na Yesu kwenda Yerusalemu kwa maisha yetu? Tuache yanayotufunga ili tuweze kumtumikia Kristo vizuri kwa uhuru wa wana wa Mungu.

Sala: Bwana! Tusaidie tuweze kuthamini uhuru wetu, tusaidie tuweze kupata uhuru kamili katika kukufuata wewe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni