Jumatano, Julai 04, 2018
Jumatano, Julai 4, 2018.
Juma la 13 la Mwaka wa Kanisa
Amo 5:14-15.21-24;
Zab 50:7-13.16-17;
Mt 8: 28-34
UTUOPOE MAOVUNI!
Watu waliokuwa na pepo wakitokea makaburini walikutana na Yesu wakati Yesu akikaribia kijiji hicho. Walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliye jaribu kupita katika njia ile. Walilia kwa sauti “una nini nasi, Mwana wa Mungu?” sehemu hii inaonesha kwamba pepo ni hatarishi na kwamba Yesu ana mamlaka makubwa. Yesu anaingia mjini kwa kuwaponya hawa watu wawili waliokuwa na pepo na hivyo kuonesha nguvu yake juu ya kuondoa uovu.
Ni wazi kwamba hawa pepo waliowashika hawa watu wawili walikuwa wakali na hivyo kufanya watu wakae kwa hofu na wasi wasi. Watu kuwa na wasiwasi kiasi kwamba hakuna mtu aliye thubutu kupita maeneo hayo. Tunaweza tusikutane na uovu kama huo mara kwa mara, lakini ni hakika kwamba tulisha kutana na uovu wakati mwingine. Muovu yupo daima na anazunguka kutafuta sehemu ya kujenga ufalme wake hapa duniani. Yesu ana mamlaka makubwa kuliko muovu. Jambo lakushangaza, aliwatoa pepo hawa na wakawaingia kundi kubwa la nguruwe na hivyo kuteremkia baharini na kufa. Watu wa mji ule wanaogopa kiasi cha kumwambia Yesu aondoke katika mji wao. Inaonekana Yesu kuwaponya hawa watu wawili ilileta mtafaruku mkubwa sana katika mji. Uovu uliojikita hauondoki kimya kimya. Kuna mahangaiko!
Watu hawa wawili walitoka makaburini , kama sisi tunavyotoka katika makaburi ya dhambi-tuliko naswa, anasa, kuhukumu kwetu wengine, dhuluma, na mitazamo yetu mibaya kwa wengine inayoleta maumivu kwa wengine. Kwasababu ya hili watu wanaweza kutuogopa sana! Lakini Yesu yupo tayari kuja kukutana na sisi sehemu tulipo. Uovu wetu humtambua Yesu na tunafanywa kuwa huru kama tukienda karibu na Yesu.
Lakini mara nyingi, Yesu anapokuja kuondoa uovu ndani mwetu, tunaweza tusitambue uponyaji. Ni mara ngapi Roho Mtakatifu anataka kutufanya upya nasi tunakataa? Tuna furahi kuishi katika hali ya dhambi na hatutaki kuacha. Hatutaki mtu atusumbue tunapo endelea kufurahia raha za ulimwengu. Tutafakari juu ya maisha yetu na kujaribu kuwa tayari katika maongozi ya Mungu na wala tusimuombe aondoke kama wale watu kwenye Injili, ili tupate kuishi katika maisha ya neema tele.
Sala:
Bwana, nisaidie niweze kubaki imara ninapo kumbana na muovu na utawala wake wa giza. Nisaidie niweze kushinda utawala wake kwa ujasiri, upendo na ukweli ili kuleta ufalme wako sehemu yake. Yesu nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni