Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Juni 29, 2018

Ijumaa, Juni, 29, 2018,
Juma la 12 la mwaka wa Kanisa.


Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume

Mdo 12:1-11;
Zab 33:2-9;
2Tim 4:6-8, 17-18;
Mt 16:13-19


MATESO YETU YA KILA SIKU YANATUSAIDIA KUKUWA KATIKA UHUSIANO NA YESU!
Watakatifu Petro na Paulo wanachukuliwa kama nguzo mbili kubwa za kanisa Katoliki lililowekwa na Kristo mwenyewe. Wote walikufa mashahidi huko Roma, wote wawili walionesha upendo wao kwa Kristo kwa kutoa maisha yao. Mt. Petro alichaguliwa na Yesu kama kiongozi wa Mitume na pia kuwa vika wake hapa duniani. Yesu alimpa ufunguo za mbinguni na mamlaka ya kuchunga kundi lake. Mt. Paulo alichaguliwa na Yesu mwenyewe wakati akielekea Dasmeski na kuwa mtume wa mataifa. Kwa jinsi Kanisa la Yesu lilivyo leo ni kwasababu ya Imani na utume waliofanya watakatifu Petro na Paulo. Ni kweli kwamba leo tuna sheherekea mitume Petro na Paulo katika Kanisa, tujaribu kujiuliza maisha yao yalikuwaje kabla?

Tuna angalia maisha ya Petro. Alikuwa mvuvi. Petro hakuwa mtu wa Imani kubwa. Leo katika Injili tunamuona Yesu akiwauliza wafuasi wake, watu wanadhani yeye ni nani? Na pia anawauliza mitume wake, na nyie mnasema mimi ni nani? Petro kwa niaba yao anajibu, “wewe ni Kristo Mwana wa Mungu aliye hai”. Ni baada ya maelezo haya Yesu anawaeleza mitume wake kuhusu mateso yake na ufufuko. Je, Petro alisema nini kuhusu hili? “…haya hayatakupata! Kamwe”. Yesu anamkemea “rudi nyuma yangu shetani!”. Hapa ndipo tunapoona kiini cha Imani ya Petro. Haikuwa sahihi. Katika sehemu nyingine wakati Yesu anatembea juu ya maji, Petro alimwambia Yesu, “Bwana, kama ni wewe uniruhusu nije kwako nikitembea juu ya maji”. Yesu alimwambia amfuate akitembea juu ya maji. Mara baada ya kutembea alianza kuzama na anamlilia Yesu amuokoe. “Ewe mwenye Imani haba, mbona uliona shaka?”. Baada ya ufufuko wa Yesu, Petro huyu huyu alikuwa mtu mwingine tofauti. Akijazwa na Roho Mtakatifu alienda huko na huko akitangaza habari njema. Imani yake sasa imekuwa yenye nguvu na imara. Tunaona pia muda wote jinsi Bwana alivyokuwa naye katika magumu yote aliyopata. Katika somo la kwanza la leo tunamuona malaika akimuokoa Petro kutoka gerezani.

Je, Paulo alikuwaje kabla? Alikuwa ni Myahudi aliyeshika sheria. Alikuwa amechukua kiapo cha kuwaangamiza waamini wote waliomwamini Yesu. Ili kutimiza haja yake alikuwa njiani akielekea Dameski akiwa njiani alitokewa na Yesu. Kukutana na Yesu huku kulimfanya Paulo awe kiumbe kipya na mtu mpya. Mtu ambaye alikuwa anataka kuwaangamiza waamini wote sasa na yeye anakuwa muamini. Anakuwa mwenye Imani kubwa kiasi cha kusema kwamba “sio mimi tena naishi bali Kristo anaishi ndani yangu” (Gal 2:20). Bwana pia alikuwa na Paulo katika magumu na mateso yake. Leo katika somo la pili linashuhudia hilo. Kwahiyo mateso haya yote walioteseka watakatifu hawa, mateso yote na manyanyaso yote waliokutana nayo hawakumwacha Bwana hata kidogo, bali walikuwa na kuongezeka sana ndani ya Bwana wao. Zaidi sana, Imani yao juu ya Mwana wa Mungu iliimarika sana. Kwa mfano wa watakatifu hawa, sisi pia tukuwe katika uhusiano wetu na Yesu Mwana wa Mungu.

Wote wawili Mt. Paulo na Mt Petro walikirimiwa kwa uaminifu wao mkubwa katika utume. Katika sherehe hii ya watakatifu Petro na Paulo, tunaomba Kristo atupe sisi wote, ujasiri, ukarimu, na hekima tunayo hitaji ili tuweze kuwa vyombo vya kufanya ulimwengu uwe huru. Kwa kuchukua mfano wa Watakatifu hawa tuweze kukuwa katika uhusiano na Yesu, Mwana wa Mungu.

Sala:
Bwana, ninakushukuru kwa zawadi ya Kanisa lako na Injili yenye kuleta uhuru linayo ihubiri. Nisaidie mimi niweze kuwa mjumbe wa ukweli huo kwa wale wote wanao uhitaji. Ninaomba tuweze kubaki tumeungana na waridhi wa mitume wako. Tuongezee uaminifu katika Injili yako. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni