Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Juni 10, 2018

Jumapili , Juni, 10, 2018,
JUMA LA 10 LA MWAKA B WA KANISA

Mwa 3:9-15
Zab 130
2 Kor 4:13—5:1
Mark 3:20-35

KUMCHAGUA MUNGU NA KUACHA DHAMBI

Siku moja kulikuwa na padre mmoja ambaye alikuwa ni mpya na alikuwa na wasiwasi sana sijui ataanzaje kufanya utume wake bila kuharibu? Akawa anawaza moyoni, sijui nifanyeje? Siku mmoja wakawa wapo katika bustani ya maua na Padre amabaye alikuwa mzee kidogo na mzoefu katika utume wake. Huyu kijana akaona kwakweli huu ndio wasaa wakumuuliza huyu mzee, nini siri ya mafanikio yake katika utume. Akamwambia yule Padre mzee. Baba nina wasi wasi sana kuhusu utume wangu, sijui watanipokeaje? Sijui nitatendaje kazi ili niweze kumpendeza Mungu na wanadamu. Yule Padre mzee akampeleka kwenye maua ya waridi akamwambia. Embu chuma ua moja hapo ambalo bado halijafunguka/halijachanua bado. Akamwambia yule Padre mdogo sasa nakuomba ujitahidi kufungua hilo ua uhakikishe linafunguka kama yalivyofunguka haya mengine na wala usiharibu hata kipande kimoja. Yule padre mdogo akatafakari akamwambia kwakweli haiwezekani, lazima naweza kuharibu sehemu na haliwezi kufunguka likiwa ndani ya mikono yangu. Basi yule Padre mzee akamwambia hata wewe utambue mambo mengine yanafanywa na Mungu, uache utume wako mikononi mwa Mungu fanya kazi yako. Mambo mengine Mungu atayafanya mwenyewe. Ukijaribu kufanya kwa mikono yako utaharibu tu. Mwenye uwezo wakulifungua ua la waridi lichanue vizuri bila kuharibika ni Mungu mwenyewe. Mkabidhi utume wako yeye atakusaidia na utachanua, lakini usipo mkabidhi ukafanya kwa nguvu zako hakika utaharibu. Duh! Yule Padre mdogo akamwambia asante Sanaa mzee wangu.

Ndugu zangu dhana ya Mwanadamu kujitegemea mwenyewe na kuacha kumtii Mungu na kuanza kufuata mashauri yake mwenyewe ndicho chanzo cha mahangaiko na kuharibu uhusiano wake na Mungu. Tunaweza kusema alitaka kufungua ua la waridi peke yake, bila Mungu na mwishowe akajikuta ameingia kwenye dhambi na kuharibu uhusiano wake na Mungu. Dhambi imeleta malumbano duniani na wala hayawezi kuisha mpaka pale tutakapo amua kumfuata Mungu, na kufufua tena uhusiano wetu naye na kumruhusu aweze kufungua maisha yetu tuchanue kama waridi. Muovu hana Nguvu kama Mungu. Yesu anatuita tuweze kuwa wanafamilia yake kwa kulishika neno lake.
Somo la kwanza linaonesha jinsi dhambi ilivyo ingia ulimwenguni. Dhambi ina leta madhara katika hali nyingi sana, mra nyingi tunalaumu wengine kwasababu ya dhambi yetu na hatukubali kupokea jukumu ya matokeo ya dhambi zetu. Mwandishi huyu wa Kitabu cha Mwanzo anaona kabisa kutakuwa na vita kati ya dhambi na watoto wa huyo mama (Eva). Dhambi itakuwepo lakini kwanjia ya Mwanamke pia wokovu utaingia ulimwenguni kumkomboa mwanadamu.
Katika somo la pili kutoka katika barua ya Kwanza kwa Wakorintho inatuambia”aliyemfufua Yesu atatufufua sisi pia na kutuweka pamoja naye katika uwepo wake” Mungu atatuweka sisi pamoja na Kristo lakini kwanza atuweke safi katika sura na mfano wake, ambayo sisi tumepoteza kwanjia ya dhambi. Maisha haya ni kumfuata tu Mungu atufanye upya daima. Tunapaswa kuwa wavumilivu. Wengi wetu tunaweza kudhani sasa tunaweza kusimama mbele ya Mungu lakini katika ukweli ni kwamba bado hatujawa na yale mapendo ya kweli ya kuweza kukutana naye. Tujitakase zaidi ili tuweze kuwa na nguvu ya kusimama mbele yake. Daima dhambi itatufanya tujifiche mbele ya Mungu kama Adamu alivyojificha katika somo la kwanza.

Injili ya Marko leo ya pekee kwani familia ya Yesu inaonesha kana kwamba Yesu amechanganyikiwa. Na inataka kuonesha Yesu amechanganyikiwa kwasababu ya yale yaliotokea hekaluni. Yesu alisema hekalu ni nyumba ya sala sio sehemu ya ulanguzi na biashara..
Inaonekana familia ya Yesu inashindwa kumwelewa Yesu lakini Yesu yupo tofauti! Yesu anatenda mapenzi ya Baba yake wala hataki kutekeleza kitu kingine kile. Majibu ya Yesu yanaonesha kuleta kitu kingine tofauti cha kuunda familia mpya ya wana wa Mungu. Wale wote ambao wanalishika neno la Mungu na kulitenda ndio kaka na dada wa Yesu. Hawa ndio wanaokaribishwa katika familia yake. Kanisa ni familia ya Yesu. Mafarisayo na Waandishi walitaka kumjaribu Yesu na hata walidhani ana pepo lakini wanaogopa kumuuliza kitu. Hawa Mafarisayo na waandishi walikosa unyenyekevu wa kujifunza kwa Yesu na hivyo kuishia kuwa na kiburi cha mioyo yao. Kwanjia nyingine hawakuwa tayari kutubu na kuachana na unafiki wao kwa njia hiyo watakufa bila kukiri dhambi zao. Na hii ndio dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu kukata tamaa na kuona Mungu hawezi kukusamehe. Kuwa na kiburi na kuacha kutubu hakika mmoja hufa katika hali ya dhambi na hivyo ni wazi hataiona Mbingu, kwani atakufa bila kuomba msamaha. Hii ndio dhambi anayokataza Yesu.

Ndugu zangu tuangalie na sisi tusije tukaingia katika kiburi cha namna hii tukashindwa kutubu dhambi zetu. Tukajiona kwamba sisi ni nani mpaka tukaungame kwa Padre? Kuwa mnyenyekevu usije ukaikosa mbingu ndugu yangu. Daima Mungu amechagua vile viumbe dhaifu ambavyo hata ulimwengu hauvidhanii na kuaibisha vyenye nguvu. Kuwa mnyenyekevu wa kukiri dhambi zako hutapoteza kitu. Hakuna aliye na ujasiri akiwa kwenye dhambi. Jiunge na Mungu utakuwa jasiri. Mungu akutunze.

Maoni


Ingia utoe maoni