Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Machi 13, 2018

Jumanne, Machi 13, 2018,
Juma la 4 la Kwaresima

Ez 47: 1-9, 12;
Zab 46: 2-3, 5-6, 8-9;
Yn 5: 1-16.


INUKA!
Leo nabii Ezekieli anatupa alama nzuri ya picha ya jinsi ya kuzaliwa upya na kuwa mpya.! Kama mfereji mdogo unaotoka katika hekalu na kuwa mto Mkubwa, ardhi kavu ya Israeli itasitawi kwa miti yenye matunda. Katika nchi ambayo daima iliteseka kwa ukame na kwa kukosa maji, sasa itasitawi, jambo hili lilikuwa la matumiani makubwa. Wakristo wa mwanzo waliamini kwa njia ya Yesu hili lilitimia. Yeye ni hekalu hai la Mungu. Yeye ni chemchemi ya maji ya uzima. Ambapo kutoka kwake miito mikubwa humwaga maji, ambapo kwa ubatizo unafanya upya ulimwengu na kuichipusha. Kanisa limeona kutoka kwa Ezekeli alama ya ubatizo. Kama vile maji ya mto huleta ukuwaji wa vitu na mengi hufanywa upya, ndivyo maji ya ubatizo yanatuletea kuzaliwa upya rohoni na kufanya yote upya tena.

Katika Injili, Yesu anamponya mgonjwa aliye pooza. Kupooza kwa mwili ni alama inayowakilisha matokeo ya dhambi. Tukitenda dhambi tunakuwa “tumepooza” sisi wenyewe. Dhambi ina matokeo katika maisha yetu na matokeo ambayo ni hakika kabisa ni kwamba tunabaki tumeanguka na tunashindwa kutembea katika njia za Mungu. Dhambi za mauti hasa, zinatufanya tukose nguvu ya kupenda na kuishi huru. Inatuacha katika mtego tukiwa tunashindwa kujali maisha yetu ya kiroho au ya wengine katika hali yeyote. Ni vizuri kuona matokeo ya dhambi. Hata dhambi ndogo inatuathiri uwezo wetu, inatukosesha nguvu, na kutuacha tukiwa vilema kwa njia moja au nyingine.

Tunapaswa kujiona wenyewe katika habari hii. Yesu hakumponya huyu mgonjwa kwa faida yake mwenyewe tu. Anamponya akitaka kutuambia kwamba anatuona katika udhaifu wetu tukiwa tunapatwa na matokeo ya dhambi zetu, anatuangalia na kutuita tuinuke tena na kutembea naye. Angalia dhambi yako, mruhusu Yesu aione, na msikilize akiongea maneno ya uponyaji na uhuru. Yesu anatupatia uponyaji kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio, hasa wakati huu wa Kwaresima. Nenda kaungame na gundua uponyaji wa Yesu. Kitubio ni jibu la uhuru unao tungoja sisi, kutufanya upya na kuwa na Baraka, neema na maisha ya mtu aliye jaa mema.

Sala:
Bwana, naomba unisamehe dhambi zangu. Ninatamani kuzifahamu nakuona matokeo yake. Ninajua unatamani daima kuniweka huru kutoka katika mizigo hii na kuiponya kutoka katika chanzo chake. Bwana, nipe nguvu niweze kuziungama dhambi zangu kwako, hasa katika sakramenti ya Kitubio. Yesu nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni