Jumapili, Machi 04, 2018
Dominika ya 3 Kwaresima
"... Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara" (Yoh. 2:16). Ni Jumapili ya 3B ya Kwaresima. Wazo kuu ni: Sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi"(Zab. 19:8). Mama Kanisa anatupatia nafasi nyingine ya kulitafakari Neno la Mungu. Katika somo la kwanza (Kut. 20:1-17), tunaletewa amri kumi za Mungu. Tunaalikwa kuzitii, kuzishika na kuziishi kama njia mojawapo ya kujitakasa. Kwaresima ndio wakati muafaka wa kufanya mazoezi ya kiroho katika kujitahidi kushika amri za Mungu tukisaidiwa na sala pamoja na mfungo. Katika somo la pili (1Kor. 1:22-25) Mt. Paulo anatukumbusha kwamba kiini chetu cha mahubiri kiwe ni "Kristu aliyesulibiwa; ...(ambaye) kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuuzi..."(1Kor. 1:23). Hata nyakati hizi zetu wapo wanaoona msalaba kwao ni kikwazo na upuuzi. Kipindi hiki cha Kwaresima ni wakati wa kuutangaza msalaba wa Kristo ambao kwetu ni nguvu na hekima ya Mungu, na kwa njia hiyo ya msalaba sisi sote tumekombolewa. Katika somo la Injili (Yoh. 2:13-26), Kristo anawafukuza wafanya biashara kutoka hekaluni, nyumba ya Mungu. Anawaambia "Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha"(Yoh. 2:18). Yesu anaelekeza hasira si kwa watu wale bali kwa kile kitendo chao cha kulinajisi hekalu; matendo yao maovu yaliyoharibu maana ya hekalu. Hasira ya Yesu haikuwa ya kulipiza kisasi bali ilikuwa ni hasira ya kuwasahihisha na kuwakumbusha wajibu wao wa kuliheshimu hekalu la Mungu, nyumba ya ibada. Hasira hii ya Yesu ilikuwa ni kuwakumbusha kile tunachoamriwa katika mojawapo ya amri kumi za Mungu "Ikumbuke siku ya sabato uitakase'(Kut. 20:8). Wafanya biashara walisahau kuitunza sabato na kuitakasa. Wakati huu wa Kwaresima tunaalikwa tutafakari yafuatayo:
Moja:Hasira zetu tunazielekeza kwa nani/nini? Kwa sababu gani nina kasirika?
Pili: Sisi pia ni hekalu la Mungu. Mt. Paulo anaandika akisema "Je, hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?"(1Kor. 3:16).Hatuna budi kuwa na heshima na mwili wetu ulio hekalu la Mungu. Mt. Paulo anatuonya tuache matendo yanayonajisi mwili/roho yetu, hekalu la Mungu. Matendo hayo ni: "Uasherati, kuabudu sanamu, uzinzi, ulawiti, wizi, uchoyo, ulevi, usengenyaji, unyang'anyi..." (Rej.1Kor. 6:9-10).Matendo haya ni biashara zinazonajisi miili yetu ambayo ni hekalu la Mungu. Hii ni Kwaresima. Tunapoanza juma la tatu, tuombe neema ya kuzishika amri za Mungu ili zitusaidie kutunza miili yetu iliyo hekalu la Mungu tukitambua kwamba "Sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi; Maagizo ya Bwana ni adili, huufurahisha moyo"(Zab.19:7-8). Ninawatakia nyote Jumapili njema. Mungu atubariki sote.
Maoni
Ingia utoe maoni