Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Februari 21, 2018

Jumatano, Februari 21, 2018.
Juma la 1 la Kwaresima

Yon 3:1-10;
Zab 51:3-4,12-13,18-19;
Lk 11:29-32

KUMKUBALI YESU NA UPENDO WAKE!
Katika masomo ya leo tunamwona Yona akipeleka Neno la Mungu kwa watu wa Ninawi, na anapo anza kuingia katika mji, anaanza kutangaza kwake kuharibiwa kwa mji huo na watu wanasikia . Mfalme anasikia na kutangaza kufunga, watu wavae magunia wajipake majivu na kutubu. Mfalme mwenyewe ana anza kuvaa magunia, kuacha kiti chake cha enzi na kukaa katika majivu. Hivyo Mungu anawaonea huruma watu wa Ninawi na ana sitisha mpango wa kuuharibu mji huo. Muujiza huu sio Mungu kuacha kuuanga miza mji wa Ninawi bali ni namna watu walivyo mgeukia Mungu. Walipokea neno la Mungu na wakaliweka katika matendo.

Katika Injili, tunaona watu ambao wanahitaji ishara ya ajabu ili waweze kusikiliza maneno ya Yesu. Yesu anashangazwa na anawaambia, Malkia wa Sheba alikuja kutoka mbali kumsikia Sulemani na Ninawi walitubu baada ya kumsikia Yona, wao wapo na mtu mkubwa zaidi kuliko Yona na Sulemani lakini wanashindwa kumtambua. Wapo na mwana wa Mungu lakini kwasababu ya mioyo yao migumu wanashindwa kumtambua Yesu nakuongoka.
Watu wakipindi cha Yesu walibarikiwa kwa kusikia neno la Mkombozi wa Ulimwengu. Je, na sisi pia?! Tuna Injili, mafundisho ya Kanisa, ushahidi wa Watakatifu wengi, uchungaji wa Baba Mtakatifu, Sakramenti na mengine mengi. tuna njia mbali mbali za kupata Injili katika Ulimwengu wa Teknologia lakini ni ajabu tunaweza kushindwa kusikia sauti ya Yesu. Tutafakari sisi wenyewe jinsi tunavyo itikia ujumbe wa Yesu. Anaongea na sisi mara nyingi kwa nguvu mbali mbali lakini tunashindwa kumsikia. Kushindwa kusikiliza, inapelekea tunashindwa kutubu.

Sala:
Bwana, unaongea nami kwa njia mbali mbali. Unahubiri kwa njia ya Neno lako, Kanisa lako na katika maisha yangu ya sala. Ninakupenda wewe, Bwana wangu mpendwa, ninatubu dhambi zangu. Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni