Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Februari 20, 2018

Somo la kwanza (Isa. 55:10-11) linaeleza nguvu ya Neno la Mungu. Kwa kinywa cha Nabii Isaya, Mwenyezi Mungu anasema kwamba kama ilivyo mvua, ambayo ikishuka kutoka mbinguni hairudi itokako, bali huinywesha ardhi, huzalisha na kuchipusha mimea, kuistawisha hata ikazaa matunda; ndivyo lilivyo Neno lake. Linatoka kinywani mwake, halirudi bure. Bali linatimiza mapenzi yake. Na litafanikiwa katika mambo yale linalotumwa kufanya. Hii maana yake ni nini? Moja, sisi ni ardhi/udongo ambao Neno la Mungu hutua. Pili, linapofika kwetu, Neno la Mungu linapaswa kurutubisha mioyo yetu. Tatu, lengo la kuturutubisha ni ili tuzae matunda. Matunda hayo hayana budi kuonekana katika maisha yetu ya kila siku. Hii ni Kwaresima. Moja ya mwaliko wa kuiishi Kwaresima ni kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu, Mtaguso wa Vatikano II unasisitiza sana juu ya kuzama katika Maandiko Matakatifu ukimwalika kila mmoja kuwa karibu na Neno la Mungu. Mtaguso unasema " Kwa hiyo makleri wote, hasa mapadre wa Kristo, mashemasi au makatekista wanaoshiriki kwa rasmi huduma ya Neno, lazima wajizamishe katika Maandiko Matakatifu kwa kuyasoma bila kuchoka na kwa makini... Watawa wajifunze "uzuri usio na kiasi kwa kumjua Kristo Yesu" (Flp 3:8) kwa kusoma mara kwa mara Maandiko Matakatifu... Lakini waamini wakumbuke kwamba kusoma Maandiko Matakatifu lazima kuwe katika mazingira ya sala, ili Mungu na binadamu waweze kuongea pamoja; kwa sababu "tunaongea tunaposali na tunamsikiliza tunaposoma Maandiko Matakatifu" (Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, ; Ufunuo, 25). Hii ni Kwaresima. Bwana Yesu anapotufundisha kumwita Mungu ni Baba katika sala ya Baba Yetu (Mt.6:9-13), hatuna budi tutambue kwamba tunamwelewa Mungu Baba na kuelewa matakwa yake kwa kulisoma na kulitafakari zaidi Neno lake, Maandiko Matakatifu kwani Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo (Mungu).

Sala
Tunakuomba ee Bwana neema ya kulishika Neno lako na kuliishi.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni