Alhamisi. 28 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Januari 28, 2018

Januari 28, 2018


DOMINIKA YA 4 YA MWAKA B WA KANISA


Kumb 18:15-20

Zab 95:1-2.6-9

1Kor 7:32-35

Mk 1:21-28


KUMSIKILIZA MUNGU

Ndugu zangu katika Kristo nguvu ya Mungu katika maisha yetu ni muhimu sana. Ni nani anaye weza kuongea na kumshinda Mungu? Je, tupo tayari kumsikiliza yeye? Tupo tayari kusikiliza kitu nje ya nafsi zetu sisi wenyewe, na kuelekea kwa nguvu kwenye utawala wa Kimungu ambaye anataka kuwasiliana na sisi,  na ambaye hutupatia uhuru wa kumchagua? Somo la kwanza leo kutoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati linatupatia mwanga kweli kweli. Watu wa Mungu wanamwambia Mungu moja kwa moja kwamba sisi hatutaki kukusikiliza wewe moja kwa moja! Na Mungu anawambia kwamba sasa watakuwa wakimsikiliza kupitia manabii. Lakini manabii wa kweli sio manabii wa uongo. 


Tunaweza kufikiri kwamba kuna kitu ambacho sio sawa kuhusu kumwambia Mungu asiongea nao moja kwa moja, lakini sisi wenyewe mara nyingi hatutaki kumsikiliza Mungu moja kwa moja kupitia neno lake, kuna wakati ambapo tunasikiliza lakini tunachagua vya kusikiliza. Hatuna tofauti na watu wakipindi cha Musa! Wakati hatutaki kumsikiliza Mungu, tunajifanya tunahitaji nabii ili tumsikilize Mungu. Tunapaswa kusikiliza neno la Mungu pia tuweze kufahamu kuhusu manabii wa uongo, neno la Mungu linatupa tahadhari juu ya manabii wa uongo na linatuonya, lakini sisi daima tunakimbilia manabii bila kulisikiliza neno la Mungu. Unapo mpa muovu awe mfafanuzi mzuri wa maandiko, atakukamata tu kama Eva alivyo mruhusu shetani amfafanulie maandiko. Siku hizi manabii wapo wengi wa kila aina, hata wengine wanatoa pepo kwa kutumia sumu ya mbu (doom au rungu), ni ajabu kweli kweli. Ni lazima kuwa makini, manabii waliowengi wapo kwa ajili ya maslahi na tena wanachagua vifungu vya mafanikio tu, na wala hawahubiri msalaba hata kidogo. Watahubiri wewe utapata gari tu, utapata nyumba na nk, hawawezi kusema jitoe ufanye kazi ili Mungu abariki kazi ya mikono yako, ni kana kwamba wanasema kama unapenda gari hili bonyeza nyota litakuwa la kwako. Lakini kiuhalisia ni kama panya anaye ngata kisigino huku akikupuliza kumbe anamaliza mguu wako. Nabii wa kweli hahubiri ili afurahishe watu tu, bali anahubiri kwasababu ndivyo Mungu anavypenda na si kwa maslahi ni ili Mungu atukuzwe na Mwanadamu apate utakatifu, je manabii wa sasa wanalenga hayo? 


Somo la pili ni kutoka katika barua ya kwanza ya mtume Paulo kwa Wakorintho. Tunaambiwa kwamba mtu ambaye hajaoa anajishughulisha na kumsikiliza Bwana. Hii haina maana kwamba mtu ambaye hajaoa ni bora zaidi kuliko wale ambao wameoa au eti kwamba Mtu ambaye hajaoa ndiye atakaye mpenda Bwana zaidi. Utakatifu wetu na thamani yetu mbele za Mungu nikufanya mapenzi yake. Na kweli baadhi ya watu ambao wameoa wanamtukuza Bwana hata zaidi ya baadhi ya ambao hawajaoa. Na ni kweli kwamba mtu ambaye hajaoa anauwezo wakuwa karibu zaidi pia na Bwana kwasababu ya ukosefu wa majukumu ya mke na watoto. Cha muhimu kwa wote ni kumsikiliza Bwana. Sisi tunaweza kuwa tumekamatwa na mambo mengi mno kiasi ambacho tunaweza kushindwa kumsikiliza Bwana. Tunasikiliza sauti ya pesa zaidi kuliko sauti ya Mungu, tunasikiliza sauti ya madaraka zaidi kuliko sauti ya Mungu, tunasikiliza sauti ya hisia za mwii zaidi kuliko kuisikiliza sauti ya Mungu ndani ya dhamiri zetu. Ukiwa hujaoa au kuolewa na hayo (pesa, madara, hisia za mwili nk.), ni wazi kwamba utakuwa mtu ambae  kweli huna sababu ya kuacha kumsikiliza  Bwana.


Somo la Injili linatuleta tena kwenye maada yetu ya kumsikiliza Bwana. Watu wanashangazwa kabisa juu ya Yesu na nguvu zake juu ya Pepo wabaya. Waliweza kuona kwamba Yesu anaongea kama mtu mwenye mamlaka yake. Lakini je, watu wainjili walimfuata Yesu? Sio kila mara! Hata wakati neno la Mungu lipo wazi mbele zetu, bado tunakuwa wagumu. Mungu ametupa sisi uhuru wa kumchangua na mara nyingi tumeishia kuchagua kumpinga, na mara nyingine hata kujipinga sisi wenyewe. Leo tusikilize nyakati nyingi ambazo Mungu anakuja kwetu. Tujitahidi kuwa waaminifu juu ya sauti ya Mungu inavyokuja kwetu katika masomo na hata tukiwa kanisani. Tuwe makini kwa ajili ya vitu vya Mungu na wakati ambapo Mungu ametutumia nguvu tuweze kuwa waaminifu. Sikiliza sauti inayo patikana katika wito wako, kama ni ndoa tii sauti ya Mungu ndani ya ndoa yako, kama ni kuhani sikiliza sauti ya Mungu ndani ya wito wako nk, usifungwe na mambo mengine ambayo yatakufanya ushindwe kuisikiliza sauti ya Mungu na kushindwa kufanya mapenzi Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni