Alhamisi, Agosti 25, 2016
Alhamisi, Agosti 25, 2016,
Juma la 21 la Mwaka
1Kor 1:1-9;
Zab 144:2-7;
Mt 24:42-51
KUWA TAYARI !
Injili ya leo inatangaza kuja sio kwa tufani bali ukombozi. Inatangaza kuja kwa Ufalme wa Mungu. Na hapo hapo tunaambiwa kwamba hatujui siku wala saa itakapokuja na kuja kwake kutakuwa kama ujio wa mwizi. Njia na silaha kubwa ya mwizi ni kuja kwakustukiza. Kuja kwa Ufalme wa Mungu hakutakuwa na kengele za tahadhari. Kuna silaha moja tuu ambayo tunaweza kuiandaa kwaujio wa ufalme wa Mungu nayo ni – kuandaa maisha yetu. Mungu ametupa sisi wanadamu uhuru wakuchagua. Kila mtu anauwezo wakuchagua jema na kutenda mema nakuishi vizuri na hapo ufalme wa Mungu ujapo atakuwa amejiandaa au mtu anauwezo wakuchagua kutenda dhambi na Mungu haingilii uhuru wake, lakini Mungu ameweka wazi njia yake kwamba kuchagua uovu sio kadiri ya sheria yake. Tuombee neema ya Mungu ili tuweze kutumia uhuru wetu vizuri tuchague kutenda mema kila wakati na tuwasaidie wengine waweze kuchagua kutenda mema ili ufalme wa Mungu ujapo kwa mara ya pili utukute tumejiandaa kila wakati.
Tuna mengi sana ya kutufundisha sisi, kila mara tunawaona vijana wadogo wanapoteza maisha wakiwa na umri mdogo kabisa, pengine kwa ajali au kwa magonjwa, tunajiuliza hivi walijua kwamba Mungu angewachukua wakiwa wadogo namna hii? Tunajiuliza hivi walikuwa wamejiandaa? Sio kazi yetu kuhukumu nakujua kuhusu wema wao lakini tunachojifuza ni kwamba siku ya mwisho ya mwanadamu hapa duniani ni Mungu mwenyewe anayepanga, lililo bora tena sana ni kuwa tayari kwa ujio wa Mungu muda wowote ule. Tukiishi kwa matumaini yetu yakiwa ndani ya Kristo, siku hiyo itakuwa ya furaha kwetu na hatutaishi kwa woga. Hofu inakuja kwasababu ya dhambi, lakini tukijipatanisha na Kristo kila mara matumaini yetu kwake ni makubwa na furaha yetu ya kuungana naye itakuwa kubwa zaidi.
Tuwasaidie ndugu zetu wote wamrudie Kristo, tukitambua kuwa hata jani la mwisho kabisa kwenye mti ni sehemu ya mti. Mkristo au ndugu unayemuona mdhambi sana bado ni sehemu ya mwili wa Kristo. Tuwasaidie ndugu zetu kwa kuwatia moyo ili wawe karibu zaidi na Kristo ili siku yake itakapokuja tuweze kupokea neema na kumlaki Kristo. Ni furaha yetu wote kwa pamoja kuuona uso wa Mungu.
Sala: Bwana, kwakupokea sakramenti kila wakati, kwanjia ya sala zangu na ndugu zangu, kwa kutembea katika mwanga wa neno lako, naomba niwe tayari daima kukupokea wewe. Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni