Alhamisi. 28 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Novemba 29, 2017

Jumatano, Novemba 29, 2017. 

Juma la 34 la Mwaka

Dan 5: 1-6, 13-14, 16-17, 23-28;

Dan 3: 62-67 (K) 59; 

Lk 21: 12-19.

 


SUBIRA, UVUMILIVU UTAKUSHINDIA MAISHA! 

Tofauti na viongozi wengine ambao ni wabinafsi ambao wanapenda kujitafutia watu wengi na wafuasi wengi, Yesu mchungaji mwema na mkweli anasema wazi kabisa kuhusu dhoruba na adha zitakazo lipata Kanisa na mengi yatakayo wapata wafuasi wake. Katika familia zetu, katika sehemu zetu za kazi, katika parokia yetu, na sehemu nyingine nyingi tuna muda mzuri wa kushuhudia thamani ya Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo. Pengine mke msumbufu nyumbani, mume asiyejali, watoto wasumbufu na wasio tii, upweke katika maisha, maisha ya kukatisha tamaa, majirani tegemezi, kutokuelewana, uhusiano uliovunjika, magonjwa, ugumu wakupata fedha, ufisadi ulio kithiri, mumonyoko wa maadili,…hali zote hizi si mateso katika ufuasi wetu? “Huu ndio wakati wakutoa ushuhuda; kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu” asema Bwana. Lakini ni nani kati yetu anayekubali kusimama pembeni na kuamua kuchagua njia wasio isafiri wengi, anayo isafiri Seremala wa Nazareti?


Kuna mambo mawili muhimu tunayopaswa kuchukuwa katika somo la Injili. Kwanza kabisa, kama Injili ya jana, Yesu anatoa unabii wa kutusaidia sisi kujiandaa kwa ujio wake. Kwa kutuambia ni nini kitakachokuja. Tutakuwa tumejiandaa vizuri wakati haya yatakapokuja. Ndio, kwa kutendewa vibaya na zaidi kabisa wale walio karibu nasi, tena hata familia na walio karibu nasi, ni msalaba mkubwa, inaweza ikatupeleka sisi katika hali ya kukata tamaa, hasira na wasiwasi. Lakini usije ukakata tamaa! Bwana aliliona hili na ametuambia tujiandae. 


Pili, Yesu anatupa jibu pale ambapo watatutenda vibaya. Anasema “kwa uvumilivu wenu mtaziokoa nafsi zenu” kwa kubaki jasiri katika majaribu ya maisha na kuwa na matumaini, huruma na ujasiri kwa Mungu tutakuwa washindi. Huu ndio ujumbe muhimu. Na huu ni ujumbe mrahisi sana kuusema bila kutekeleza.


Tafakari leo juu ya wito wa Yesu anaotupa kuhusu kuvumilia. Mara nyingi wakati uvumilivu unavyo hitajika, mara nyingi tunajisikia kama tujibu, kupigana na kuwa na hasira. Lakini wakati mambo yanavyokuwa magumu tunajikuta tukiishi injili kwa karibu zaidi kuliko kipindi kingine pengine cha furaha. Mara nyingi zawadi ambayo tunaweza kupewa ni kwa kile ambacho ni kigumu zaidi, kwasababu kinabeba fadhila hii ya uvumilivu. Kama unajikuta katika hali hizo leo hii, fungua macho yako kwenda kwenye matumaini kuhitaji fadhila hii. 


Sala:

Bwana, ninakupa wewe misalaba yangu, maumivu na mateso. Ninajikabidhi kwako katika hali ambazo nimeumizwa. Katika majeraha madogo, ninaomba msamaha. Na wakati chuki ya wengine inanifanya mimi niumie, ninaomba niweze kuvumilia katika neema yako. Yesu, nakuamini wewe.

Amina


Maoni


Ingia utoe maoni