Jumamosi, Agosti 20, 2016
Jumamosi, Agosti 20, 2016,
Juma la 20 la Mwaka C wa Kanisa
Kumbukumbu ya Mt. Bernard, Abbate na Mwalimu wa Kanisa.
Ez 43:1-7;
Zab 84:9-14;
Mt 23:1-12
MWALIMU MMOJA!
Ujumbe wa Injili ya leo unaanza na maneno makali kabisa kuhusu Mafarisayo na Wanasheria. “Walimu wa sheria na Mafarisayo wamekalia kiti cha Musa. Fanyeni yote wanayo waambia bali msifanye wanayotenda”, “hawatendi wanacho hubiri”. Kushindwa kutenda tunacho hubiri ni bahati mbaya Sanaa. Ni kweli kwamba makuhani na watawa wanachukua nafasi ya Musa. Tunapaswa kutoa ushuhuda wa Kristo kwa matendo yetu alafu maneno yafuate. Wazazi wanapaswa wawafundishe watoto wao kwanza, kwa mifano ya maisha yao, na hapo huenda hata maneno yasiwe ya lazima. Vijana wadogo wanavutwa sana na mawasiliano kwa njia ya matendo kuliko maneno matupu. Mt. Fransisko wa Assis aliwaambia ndugu zake, ‘hubirini na pale inapo bidi tumia maneno’. Akimaanisha kwamba hata muonekano wa mtu na matendo yake ni mahubiri tosha, haitaji hata kusimama na kupaza sauti, ahubiri tuu kwa maneno pale inapolazimu. Pengine tujiulize, je uwepo wetu mahali Fulani unahubiri chochote? Watu wakikuona wanamuona nani? Unapoingia ofisini wakati wa kazi asubuhi watu wanamuona Yesu aliyeleta faraja au wanatamani uumwe ubaki nyumbani? Maisha yetu yanapaswa kutoa ujumbe wa Amani na faraja watu wanapotuona. Tufikie mahali hata tukifika mahali licha ya wanadamu tu, hata viumbe vyote vinapata Amani tunapotokea.
Hapa swali linakuja: je, kwasababu wahubiri hawatendi wanayosema je, wanaohubiriwa wasitende kwababu wahubiri wenyewe hawatendi? Jibu la Yesu ni kwamba Fanyeni wanayo waambia, lakini msifanye wanayotenda. Kwamfano mmoja anaweza kusema, mimi siendi kuungama, kwani mimi sio mwema kuliko hao mapadre? Yesu angejibu hivi, kwanza kabisa mimi ndiye ninaye hukumu na kujua ni nani aliye mwema, pili, ni mimi niliyewapa mamlaka yakuwaondolea watu dhambi, unaweza ukuwa mwema zaidi kuliko wao baada yakupokea maondoleo ya dhambi kutoka kwao.
Zaidi sana katika Injili ya leo, Yesu anatuambia sisi wote tuna Baba mmoja na Mwalimu mmoja. Kwanini Yesu ndiye mwalimu mmoja? Ni kwasababu yeye ni Ukweli. Hakuna mwalimu mwingine anayeweza kusema yeye ni ukweli. Ukweli unaotangazwa na wale waliokalia kiti cha Musa, sio kutoka kwao wenyewe. Makosa wanayofanya viongozi ni kutoka kwao wenyewe. Ukweli wanaotangaza viongozi ni kutoka kwa Kristo, ambaye ni ukweli, ambaye kama tulivyoona anawaambia fanyeni wanayo waambia. Kwasababu wanachukua nafasi ya Musa, wanatangaza sheria ya Mungu. Lakini msifanye wanayotenda kama hawafuati sheria wanayohubiri. Tusisahau pia kila mmoja wetu ni mwalimu kwa namna yake, kama mweyekiti wa jumuiya, kijiji, uongozi serikalini, wazazi nk, lazima maisha yetu bila hata kusema yatoe ujumbe na ukweli wa Kristo. Tuombee neema hiyo, tutende kadiri ya sheria ya Kristo. Na sheria ya kristo ni Upendo kwa Mungu na jirani.
Sala: Nifundishe Yesu, kwanjia ya Roho wako Mtakatifu. Nishike mkono na uniongoze. Amina
Maoni
Ingia utoe maoni