Alhamisi, Septemba 07, 2017
Alhamisi, Septemba 7, 2017.
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa
Sala ya Kanisa (Zaburi)-Juma la 2
MASOMO YA MISA
Kol 1: 9-14;
Zab 98: 2-6;
Lk 5: 1-11
NGUVU YA NENO LA YESU!
Tumesikia juu ya nguvu ya maneno ya Yesu juma hili. Katika Injili, tunamuona Petro na wenzake walikuwa na bahati mbaya kwamba hawakupata samaki usiku uliopita. Yesu anamwambia tena Petro achukue jarife baharini kwa mara nyingine na atupe nyavu ili kuvua samaki. Petro anajibu kwamba “tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha tusipate kitu, lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu kwa mara nyingine”. Kiasi cha samaki wengi waliovua kiliwashangaza sana. Ilimshtua Petro, alihisi uwepo wa utukufu wa Mungu. Alianguka magotini pa Yesu kwa kujitambua kutoka ndani kutokustahili kwake, “ondoka kwangu” alisema, “kwakuwa mimi ni mtu mwenye dhambi”. Kumbukumbu ya tukio hili halikuisha katika maisha ya Petro katika kumfuasa Yesu, lilileta msukumo wa ndani na imani kubwa ndani yake juu ya Yesu. Petro aliandaliwa kwani alikuwa afanye jambo kubwa kwa ajili ya Yesu “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Yesu anatuita nasi leo, pengine mpaka sasa hatujafanya kitu kwa ajili ya faida ya roho zetu. Pengine tumejaribu kushusha neti, kwakuishi maisha yetu bila Yesu na mwisho hatujapata kitu, pengine tumetegemea nguvu zetu wenyewe na mwishowe tumeishia bila chochote. Pengine kwa maisha yetu tumeshindwa kuwavua watu waje kwa Yesu kwasababu ya maisha yetu ya ubinafsi.
Licha ya yote haya Yesu leo anatupa tena nafasi nyingine tutupe tena nyavu zetu, tumrudie tena yeye, kama tulizoea kuishi maisha bila neno lake basi tuanze leo kuliishi tena, tutavua samaki wengi zaidi, tutafanikiwa sana maisha yetu kama Yesu atatawala nasi daima. Kwa maisha yetu tutakuwa kivutio cha kuwaleta wengi kwa Yesu. Maisha yetu yakitawaliwa na Yesu wengi watavutwa nasi na kwa pamoja tutakuwa wavuvi wawatu tunaowaleta watu kwa Yesu ili kwa pamoja tumtumikie yeye.
Sala. Bwana, natamani tena kurusha jarife nikiwa na neno lako ili niweze kutangaza katika njia uliyo niitia. Nisaidie mimi kusema “NDIO” kwako katika mambo yote. Yesu nakuamini wewe. Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni