Jumatatu. 13 Mei. 2024

Tafakari

Ijumaa, Agosti 12, 2016

Ijumaa, Agosti 12, 2016,
Juma la 19 la mwaka C wa Kanisa

Ez 16: 1-15, 60, 63;
Is 12: 2-6;
Mt 19: 3-12

NDOA-AGANO LA UPENDO!

Katika somo la Injili leo tunaona tafakari na ukweli kuhusu ndoa na maisha ya kitawa. Yesu anaeleza kuhusu kifungo cha ndoa. Mtu yeyote asitenganishe- mtu anayeongelewa hapa ni mwanamume sio mtu mwingine wa tatu kama hakimu hivi. Katika ndoa za Wayahudi ilikuwa ni mkataba, ambao mwanamume alikuwa na uwezo wakuuvunja (Kumb 24:1). Mafarisayo waliichukua sheria hii kama sheria nzuri, bali Yesu katika Injili anaielewa kama sheria iliowekwa kwa wale waliokuwa na mioyo migumu. Anawaeleza akiwarudisha kabisa mwanzoni mwa mpango wa Mungu kuhusu ndoa aliokuwa nao tangu kuumbwa kwa Ulimwengu, “Kwahiyo Mwanamume atamuacha Baba yake na Mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja’” (Mwanzo 2:24)

Siku hizi uelewa kuhusu ndoa, talaka na maisha ya usafi wa moyo unapata maana mbali mbali. Kizazi cha sasa imewawia vigumu kuelewa kwamba ndoa ni kifungo na Agano la maisha yote. Wakati watu wanapofikiria hivyo wanaona haifai na haiwezekani na wanamua kupeana talaka kama njia rahisi tu. Kuishi katika mahusiano bila ndoa inawavutia vijana wa leo zaidi kuliko kufunga ndoa kwani wanaona ni rahisi zaidi kuachana kama maisha hayaendi. Watu wanaishi uchumba sugu miaka baada ya miaka hata wengine wamefariki wakiwa katika hali hiyo. Leo tunaalikwa tusikie ujumbe wa Yesu ambao ni changamoto kwetu. Hakuna maisha ya majaribio katika ndoa, ndoa ni agano kati ya mume na mke, na linafanyika kwa uhuru kamili wa mke na mume bila shuruti, baada ya maamuzi yao hufanya agano hilo hadharani na kuamua kuishi pamoja siku zote za maisha yao. Tofauti na hilo sio ndoa ni maisha ya dhambi na kuigiza.

Sala: Mungu Baba yetu, tunaomba ulichokiunganisha wewe Mwanadamu asikitenganishe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni