Alhamisi. 28 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Agosti 31, 2017

Alhamisi, Agosti 31, 2017
Juma la 21 la Mwaka

Sala ya Kanisa (Zaburi) - Juma 1
___________________

MASOMO YA MISA
1 Thes 3: 7-13;
Zab 89: 3-4, 12-14, 17;
Mt 24:42-51
___________________

KUWA TAYARI KUKUTANA NA BWANA!

Injili ya leo inatangaza si kuja kwa ghadhabu bali ukombozi. Inatangaza kuja kwa ufalme wa Mungu. Hatujaambiwa ni lini, ila hatujui siku wala saa ya kuja kwake, kuja kwake kunafananishwa na kuja kwa mwizi. Silaha moja wapo ya mwizi ni kuja kwa kushtukiza. Hivyo kuja kwa Ufalme wa Mungu hakutakuwa na kengele za tahadhari. Kuna silaha moja ambayo tunaweza kuitumia kujiandaa kwa kuja kwa ufalme wa Mungu nayo ni “kujiweka tayari daima” katika maisha yetu ya kila siku.

Hivi ingekuwa leo ndio siku yenyewe ingekuwaje? Hivi ingekuwaje kama ulikuwa unaifahamu hiyo siku ya kuja kwake Mwana wa Adamu ulimwenguni ya kuwahukumu wazima na wafu? Je, ungeanza kutenda tofauti? Je, ungejibu nini kwa swali hilo?

Kama tunataka kujibu swali hilo vizuri, tunapaswa kuishi kila siku vizuri kana kwamba ndio siku yetu ya mwisho ya kuishi hapa dunia. Lakini huu wito wa kuwa tarayari una maana zaidi ya kusubiri mwisho wa kuja Kristo. Ina maana ya kila wakati anapokuja Bwana wetu katika hali ya neema. Inaonesha uwepo wa upendo na huruma ya Mungu katika mioyo yetu. Ina leta maana ya wito wake wa kila siku wa kuwa karibu naye.

Je, upo makini kumsikiliza siku hizi anavyo kuja kwetu kila siku? Je, upo tayari katika hali zote ambazo Mungu anatamani kuja kwetu katika hali mbali mbali? Ingawaje hatujui siku ya kuja kwake Bwana wetu katika utukufu wote? Ingawaje hatujui siku atakapo kuja katika utukufu wote siku ya mwisho, tunatambua kwamba kila siku ni siku ya kuja kwa neema yake. Msikilize yeye kwa makini, kuwa makini na kuwa tayari!

Sala: Bwana, nisaidie niweze kutafuta sauti yako na kuwa imara katika kusikiliza uwepo wako katika maisha yangu. Ninaomba niwe tayari daima na kukusikiliza wewe unapo niita. Yesu nakutuamini wewe. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni