Jumamosi, Agosti 26, 2017
Jumamosi, Agosti 26, 2017
Juma la 20 la Mwaka
___________________
Rut 2: 1-3, 8-11, 4: 13-17;
Zab 128: 1-5 (R) 4;
Mt 23: 1-12.
___________________
UHUSIANO KATI YA MANENO NA MATENDO!
Jumamosi katika utamaduni wa Kanisa ni siku iliyowekwa kwa ajili ya kumkumbuka Mama yetu Bikira Maria. Maria alikuwa mnyenyekevu kuliko kitu chochote. Alizaliwa bila dhambi ya Asili, mkamilifu katika hali zote. Alibeba kila fadhila ndani ya roho yake. Yeye ni Eva mpya, Mama mpya wa watu wote wanaoishi. Na Yeye ameheshimiwa na kuwa Malkia wa mbingu na nchi. Alikuwa na kila sababu ya kujiinua juu na kuheshimiwa na wanadamu wote katika maisha yake. Lakini kwa unyoofu na unyenyekevu wake hakufanya hivyo. Yeye mwenyewe alijishusha na hata kuwa chini. Lakini kwa milele yote Mungu amemuinua juu. Anaonekana Malkia atapendwa na kuheshimiwa na wote. Fadhila zake zote zitana nyanyuliwa na kuonekana na wote waweze kujifunza.
Ujumbe wa Injili ya leo unaanza na maneno makali kabisa kuhusu Mafarisayo na Wanasheria. “Walimu wa sheria na Mafarisayo wamekalia kiti cha Musa. Fanyeni yote wanayo waambia bali msifanye wanayotenda”, “hawatendi wanacho hubiri”. Kushindwa kutenda tunacho hubiri ni bahati mbaya Sanaa. Ni kweli kwamba makuhani na watawa wanachukua nafasi ya Musa. Tunapaswa kutoa ushuhuda wa Kristo kwa matendo yetu alafu maneno yafuate. Wazazi wanapaswa wawafundishe watoto wao kwanza, kwa mifano ya maisha yao, na hapo huenda hata maneno yasiwe ya lazima. Vijana wadogo wanavutwa sana na mawasiliano kwa njia ya matendo kuliko maneno matupu. Mt. Fransisko wa Assis aliwaambia ndugu zake, ‘hubirini na pale inapo bidi tumia maneno’. Akimaanisha kwamba hata muonekano wa mtu na matendo yake ni mahubiri tosha, haitaji hata kusimama na kupaza sauti, ahubiri tuu kwa maneno pale inapolazimu. Pengine tujiulize, je uwepo wetu mahali Fulani unahubiri chochote? Watu wakikuona wanamuona nani? Unapoingia ofisini wakati wa kazi asubuhi watu wanamuona Yesu aliyeleta faraja au wanatamani uumwe ubaki nyumbani? Maisha yetu yanapaswa kutoa ujumbe wa Amani na faraja watu wanapotuona. Tufikie mahali hata tukifika mahali licha ya wanadamu tu, hata viumbe vyote vinapata Amani tunapotokea.
Hapa swali linakuja: je, kwasababu wahubiri hawatendi wanayosema je, wanaohubiriwa wasitende kwababu wahubiri wenyewe hawatendi? Jibu la Yesu ni kwamba Fanyeni wanayo waambia, lakini msifanye wanayotenda. Kwa mfano mmoja anaweza kusema, mimi siendi kuungama, kwani mimi sio mwema kuliko hao mapadre? Yesu angejibu hivi, kwanza kabisa mimi ndiye ninaye hukumu na kujua ni nani aliye mwema, pili, ni mimi niliyewapa mamlaka yakuwaondolea watu dhambi, unaweza ukawa mwema zaidi kuliko wao baada yakupokea maondoleo ya dhambi kutoka kwao.
Zaidi sana katika Injili ya leo, Yesu anatuambia sisi wote tuna Baba mmoja na Mwalimu mmoja. Kwanini Yesu ndiye mwalimu mmoja? Ni kwasababu yeye ni Ukweli. Hakuna mwalimu mwingine anayeweza kusema yeye ni ukweli. Ukweli unaotangazwa na wale waliokalia kiti cha Musa, sio kutoka kwao wenyewe. Makosa wanayofanya viongozi ni kutoka kwao wenyewe. Ukweli wanaotangaza viongozi ni kutoka kwa Kristo, ambaye ni ukweli, ambaye kama tulivyoona anawaambia fanyeni wanayo waambia. Kwasababu wanachukua nafasi ya Musa, wanatangaza sheria ya Mungu. Lakini msifanye wanayotenda kama hawafuati sheria wanayohubiri. Tusisahau pia kila mmoja wetu ni mwalimu kwa namna yake, kama mweyekiti wa jumuiya, kijiji, uongozi serikalini, wazazi nk, lazima maisha yetu bila hata kusema yatoe ujumbe na ukweli wa Kristo. Tuombee neema hiyo, tutende kadiri ya sheria ya Kristo. Na sheria ya kristo ni Upendo kwa Mungu na jirani.
Tutafakari leo sisi ni akina nani? Je, sisi tunajinyanyua kama Mafarisayo wanaopenda kuheshimiwa tu? Au sisi tupo kama Mama yetu Bikira Maria aliye tawaliwa na unyenyekevu wa hali ya juu? Chagua kuishi kama Mama Maria na Mungu atakubariki daima. Unyenyekevu huja kabla ya heshima.
Sala: Bwana, ninakuomba nione uzuri na wema wa Mama yako Maria. Ninakuomba nimpende na kumpa heshima. Na kwa upendo huo na heshima ninakuomba nimuige yeye katika kuishi katika kila njia. Yesu nakuamini wewe. Amina
Maoni
Ingia utoe maoni