Alhamisi. 28 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Agosti 20, 2017

Jumapili, Agosti 20, 2017
Juma la 20 la Mwaka
___________________

Is 56:1, 6-7;
Zab 66:2-3, 5-6, 8;
Rom 11: 13-15, 29-32;
Mt 15:21-28
___________________

KWA IMANI, SISI WOTE WATOTO WA MUNGU


Masomo ya leo yanaonesha hali ya ajabu ya jinsi Mungu anavyotoa wokovu wake kwa watu wote. Yesu alikuja kuwapa watu wote mapendo na wote wanaitwa kuwa wafuasi wake. Kama Wakatoliki sisi tumejikita katika ukristo ambao unatolewa kwa wote, na unapatika kwa wote wale wanaopenda. Neno “Katoliki” ni neno walilopewa wakristo wa kwanza baada ya kutambulika kwamba wanakaribisha watu wote bila ubaguzi. Mt. Inyasi wa Antokia alisema “Sehemu yeyote alipo Kristo, kuna Kanisa Katoliki”.

Hofu ya kupoteza Taifa lao na utambulisho wa dini yao umeifanya Israeli kujitenga na watu wengine na kuwa na sheria kali kuhusu watu wa njee. Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kinasema “usifanya agano na wao wala usiwe na huruma na wao…msioane nao, wala kuwapa mtoto wako aolewe nao wala kijana wako kuchukua mke huko kwasababu watafanya watoto wenu waabudu miungu mingine”(Kumb 7:2-4). Kinyume na hilo, somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya, “katika nyumba ya Mungu hakuna aliye mgeni”. Wimbo wa katikati unabeba maada hiyo hiyo kwakusema kwamba “Mkono wa Mungu wa kuokoa utaonekana na ‘mataifa yote’ ”. Paulo pia aliezea pia hili alipo Sali “mataifa yote watakuja kuuona utukufu wa Mungu uliofunuliwa na sura ya Yesu (1Kor 4:6). Katika somo la pili Paulo, ana wahakikishia wasomaji wake kwamba ‘Mungu anataka kuwaonesha watu wote huruma yake’(Rom 11:32).

Wakristo wa kwanza walikutana na hali ya utengano kuhusu Wayahuni na Wayunani. Na ilisemwa kuwa Injili ilikuwa ihubiriwe kwa wa Israeli tu. Ili kuongezea chumvi usemi wao wali rejea utume wa Yesu (Mt 10:5-6). Kwasababu ya muda mfupi Yesu alikita utume wake kwa “kondoo waliopotea wa nyumba Israeli.”

Katika somo la Injili Yesu anafuatwa na mwanamke Myunani, aliyeomba msaada kwa Yesu kwasababu ya mtoto wake aliyekuwa amepagawa na pepo mbaya. Jinsi, Yesu alivyo kabiliana na mwanamke huyu inaleta maana, kwamba Wayunani hawatatengwa na waisraeli. Mwanamke huyu amekuwa mfano wa Imani kuu. Kwasababu ya Imani yake Mama huyu ameweza kushinda jaribu la Yesu. Alishinda kwa kuwa na Imani kubwa. Alitambua kuwa hana sehemu nyingine zaidi ya Yesu. Na hivyo alijikita kwa mmoja tu amabaye angeweza kumsaidia. Hili lilikuwa ni tendo lake la Imani.
Ingaweje Yesu alijibu ombi lake katika hali ambayo ni ya kushangaza kidogo “Mimi nilitumwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli”. Aliongea naye katika lugha ambayo Mwanamke yule aliweza kuelewa wengine hawakuweza kuielewa. Yesu anatumia picha ya “kundi la kondoo” ambapo neno hili lilitumika mara nyingi katika Agano la Kale. “Ni mimi mwenyewe nitawachunga kondoo wangu….nitawachunga kondoo wangu kwa haki” (Ez 34:11-16). Yesu kwakusema yeye ni Mchungaji wa Israeli, Yeye anakamilisha unabii huo na mwanamke huyu anaelewa. Anatambua kuwa yeye si mmoja wao kati ya wale waliochaguliwa. Lakini anajinyenyekesha magotini kwa Yesu, akiomba “Bwana, nisaidie” .

Yesu anajibu katika hali ya lugha ya ukali ya Wayahudi “sio vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwapa mbwa”. Waisraeli walikuwa ni kondoo. Kumuita mtu “mbwa” ni hali ya ukatili na dharau ambayo waisraeli waliwapa wapagani (Mt 7:6, Rev 22:15, FIl 3:2). Kutoka katika midomo ya Yesu, maneno haya yanashangaza, na hasa ikitegemea mwanamke huyu alimwendea Yesu kwa heshima kubwa. Mara tatu akimwita “Bwana”.

Ufunguo wa kuelewa mazungumzo haya nikutazama matokeo ya mwisho. Yesu alimpa mwanamke huyu muda wakuonesha Imani yake kwa watu wote. Maneno yake yalimfanya yeye angare kwa wote. Mwanamke huyu alionesha Imani yake ndio maana hata sasa tunashuhudia Imani yake na unyenyekevu wake. Mwanake huyu hakuona shida kuitwa “mbwa”. Hakujisikia kwamba yeye asiye thaminika. Alidhihirisha kuwa “mbwa” mwaminifu anaye mpenda na kumtiii Bwana wake. Kwa kuonesha Imani hii, ilimfanya Yesu atende muujiza ule ambao alitaka kumtendea. Mwanamke huyu Mkananayo anachukuliwa kama kioo kizuri cha Imani. Alitambua kwamba yeye hastahili kitu, kuamini tu katika neno la Yesu aliingia katika wokovu. Alishikilia hilo na kuliweka kama zawadi.

Je, sisi ni watoto waaminifu wa Baba yetu wa mbinguni? Je, tupo tayari kusema kama yule mwanamke kwenye Injili,? Je sisi ni watii kama mbwa mbele ya bwana wao? Mara nyingi sisi tupo katikati na pia tunapenda kujitenga. Tujifunze kutoka katika hali hii ya Yesu kukutana na mwanamke huyu, na hivyo tuweze kuwa watoto wa Mungu. Kwani Mt. Paulo anasema wazi kwamba “Katika Kristo, sisi wote ni watoto wa Mungu kwa njia ya Imani…au sisi wote ni wamoja katika Kristo” (Gal 3:26-29).

Sala: Bwana, ninatambua kwamba mimi sistahili huruma yako kila siku katika maisha yangu. Lakini pia ninakiri kwamba wewe una huruma ambayo ni zaidi hata ya ile ninayo tamani uweke ndani mwangu, mimi maskini na mdhambi mkubwa. Ninakuomba huruma hiyo Bwana wangu, ninaweka Imani yangu yote kwako. Yesu, nakuamini wewe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni