Alhamisi. 28 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Agosti 18, 2017

Ijumaa, Agosti 18 2017
Juma la 19 la Mwaka

Yos 24:1-13
Zab 135:1-3, 16-18,21-22,24
Mt 19: 3-12


NDOA-AGANO LA UPENDO!

Katika somo la Injili leo tunaona tafakari na ukweli kuhusu ndoa na maisha ya kitawa. Yesu anaeleza kuhusu kifungo cha ndoa. Mtu yeyote asitenganishe- mtu anayeongelewa hapa ni mwanamume na mwanamke sio mtu mwingine wa tatu kama hakimu hivi. Katika ndoa za Wayahudi ilikuwa ni mkataba ambao mwanamume alikuwa na uwezo wakuuvunja (Kumb 24:1). Mafarisayo waliichukua sheria hii kama sheria nzuri, bali Yesu katika Injili anaielewa kama sheria iliowekwa kwa wale waliokuwa na mioyo migumu. Anawaeleza akiwarudisha kabisa mwanzoni mwa mpango wa Mungu kuhusu ndoa aliokuwa nao tangu kuumbwa kwa Ulimwengu, “Kwahiyo Mwanamume atamuacha Baba yake na Mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja’” (Mwanzo 2:24)

Ndoa ni nini? “tangu mwanzo Mungu aliwafanya Mwanamume na Mwanamke…” kwahiyo tangu Mwanzoni Mungu alitegemea Muunganiko Mtakatifu wa ndoa. Ndoa ni fumbo kweli. Kila mtu ni fumbo na muunganiko wa watu wawili (mke na mume) ni fumbo kubwa zaidi. Kama fumbo kila mmoja anapaswa kuingia kwa uwazi na unyenyekevu mkubwa huku akisema “Ninataka kukujua wewe zaidi na zaidi kila siku”. Kila mtu ambaye umemjua na kuwa mke au mume ni fumbo nzuri la utukufu wa uumbaji wa Mungu ambaye unaitwa sio kwenda kumjaribu bali kuigia katika undani wa ndani kila siku. Unyenyekevu unasaidia wanandoa kuwa wazi juu ya kila mmoja kila siku katika hali mpya ili kuelendelea kutambua zaidi ndani ya kila mmoja uzuri uliyo ndani ya kila mmoja, ili kutimiza kazi yao ya kuwa wamoja. “sio wawili tena, bali mwili mmoja”. Ni wachache sana wanaofahamu maana ya hili na niwachache sana wanaoingia katika undani huu wa maana halisi ya wito wa ndoa.

Siku hizi uelewa kuhusu ndoa, na maisha ya usafi wa moyo unapata maana mbali mbali. Kizazi cha sasa kimewawia vigumu kuelewa kwamba ndoa ni kifungo na Agano la maisha yote. Wakati watu wanapofikiria hivyo wanaona haifai na haiwezekani na wanaamua kupeana talaka kama njia rahisi tu. Kuishi katika mahusiano bila ndoa inawavutia vijana wa leo zaidi kuliko kufunga ndoa kwani wanaona ni rahisi zaidi kuachana kama maisha hayaendi. Watu wanaishi uchumba sugu miaka baada ya miaka hata wengine wamefariki wakiwa katika hali hiyo. Leo tuna alikwa tusikie ujumbe wa Yesu ambao ni changamoto kwetu. Hakuna maisha ya majaribio katika ndoa, ndoa ni Agano kati ya mume na mke, na linafanyika kwa uhuru kamili wa mke na mume bila shuruti, baada ya maamuzi yao hufanya Agano hilo hadharani na kuamua kuishi pamoja siku zote za maisha yao. Tofauti na hilo sio ndoa ni maisha ya dhambi na kuigiza.

Tafakari leo kuhusu mtu ambaye yule umeitwa kumpenda hasa mwenzako wa ndoa, kumuita mwenzako ni fumbo, ni hatua ya kwanza kabisa ya kuleta furaha ya kutambua kwamba huwezi kumfahamu kwa kila kitu. Lakini kwa kutambua uzuri wa “fumbo” hili litakuongoza kujifunza upekee wa mwenzako na kujifunza kwa unyenyekevu wito wa umoja wa kibinadamu, hasa katika ndoa.

Sala: Bwana, ninaomba unisaidie niweze kuona uzuri wa fumbo la watu ulioweka katika maisha yangu. Nisaidie mimi niweze kuwapenda kwa unyenyekevu. Nisaidie mimi niweze kuwa na upendo zaidi kwa mke/mume wangu kila siku. Yesu nakuamini wewe. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni