Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Agosti 09, 2016

Jumanne, Agosti 9, 2016,
Juma la 19 la Mwaka
Kumbukumbu ya Mt. Teresia Benedikta wa Msalaba, Bikira na Shahidi

Ez 2:8 -3:4;
Zab 119:14, 24, 72, 103, 111, 131;
Mt 18: 1-5, 10, 12-14


NI NANI MKUBWA KATIKA UFALME WA MUNGU?

Kuna video katika mitandao inayohusu Matt Woodrum, ambayo inabeba jina la “Kijana mlemavu awavutia wengi nyakati za mwisho”. Huyu kijana Matt ilikuwa vigumu kwake kutembea, lakini alishiriki katika mashindano ya kukimbia (katika mzunguko wa duara). Wakati mashindano yalipoanza wakimbiaji wote walimpita nakukimbia nakumaliza. Wakati akiwa nusu ya mzunguko wale wakimbiaji wengine walishamaliza mzunguko mwingine nakumpita. Na wakati hajamaliza mzunguko wa kwanza wote wakamaliza mizunguko yote. Lakini Matt hakuacha kuendelea kuzunguka, hata yule kiongozi wake alivyomwambia aache yeye hakuacha. Alisema anataka kumaliza. Hakujali ni sehemu ghani yeye alitaka kumaliza. Watu kwakuona moyo wake, wakamzunguka na kuanza kumpigia makofi nakusema “songa mbele, songa mbele Matt” Matt aliwafundisha wote somo. “Kushinda haimaanishi kumaliza kwa mwendo uliopangwa”

Katika somo la Injili tunaona wafuasi wa Yesu wakimuuliza; ‘ni nani aliyemkubwa katika Ufalme wa mbinguni?’ Matt, anatupa jibu, yule mdogo, mnyonge, anayeonewa, aliyekama mtoto, asiyejiweza………Wale waliojawa na elimu ya juu kabisa, matajiri na wenye mamlaka, wakialikwa kwenye sherehe kwanza wanaangalia ni nani atakuwepo ili kusimamia shughuli zake? Pia nitakuwa katika sehemu ghani kati ya waalikwa? Je nitapewa heshima ghani? Wakati kama mtoto, au mlemavu angealikwa kwa sherehe hiyo, angejisikia mwenye bahati sana kualikwa kwenye sherehe kama hiyo. Wanatambua kwakweli hawastahili kwa mwaliko huo, lakini wamealikwa na Bwana wa sherehe.

Wafuasi nao wameanguka kwenye mtego wakudhani kwamba wanastahili kwenye Ufalme wa Mungu. Kwamba ni haki yao kuwa pale, na kuwa katika nafasi ya juu kabisa. Wakati watoto hawajui hata kama watashiriki katika Ufalme huo. Wafuasi walikosa unyenyekevu, walipoteza maana ya maisha yao nakujisahau wao ni nani. Je, mimi na wewe tupo je? Je, unafikiri una haki ya kuwa katika Ufalme wa Mbinguni? Je, unasubiria sehemu ya juu kwasababu ya utume unaofanya kwaajili ya Mungu? Kama unataka kuingia katika Ufalme wa Mungu, kuwa na moyo mnyofu kama wa watoto. Tunapaswa kuwa na moyo mnyofu uliojaa unyenyekevu ili tuyapokee vyema mapenzi ya Mungu, kwa namna hii bila hata mastahili yetu, twajuaje kama Mungu hatatukaribisha kwake? Daima tuombee neema hiyo.

Sala: Bwana, fanya moyo wangu uwe mnyenyekevu na mnyoofu kama wako. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni