Jumatatu, Julai 31, 2017
Jumatatu, 31 Julai, 2017,
Juma la 17 la Mwaka
Kumbukumbu ya Mt. Inyasi wa Loyola,
Kut 32:15-24,30-34
Zab 106:19-23 (k) 1
Mt 13:31-35
UKUBWA MACHONI MWA MUNGU
Yesu akiongea kuhusu Ufalme wa Mungu alisema, “Ufalme wa Mungu upo pamoja nanyi” (Lk 17:21). Tunaitwa leo kuendeleza kazi hii ya Ufalme wa Mungu. Tunaweza kuwa na ugumu tuanzie wapi. Yesu anatuambia kwamba hata mbegu ndogo kabisa ya haradali inakuwa na kuwa mti mkubwa. Ni sawa sawa na kitendo kidogo kabisa chaweza kukuza Ufalme wa Mungu. Kwasababu Ufalme wa Mungu upo kati yetu, tunapaswa kuanza kutenda kadiri yake. Tukiwa tunaacha njia za uovu, mawazo mabaya na kugeukia njia ya haki, inaweza ikawa hatua ndogo. Kitendo hiki kidogo chaweza kukuwa na kuwa mti mkubwa ambapo ndege wa angani hupata pumziko. Kitendo kidogo katika familia yangu chaweza kukuza familia yangu na kuwa sehemu kubwa ya kushuhudia kueneza Ufalme wa Mungu. Kitendo cha ukarimu kwa jamii, chaweza kubadilisha jamii nzima na kufanya Ufalme wa Mungu kuenea kama moto mkubwa.
Mara nyingi tunafikiria kwamba maisha yetu sio muhimu sana kama ya wengine. Tunaweza kuwaangalia watu wengi walio endelea na walio maarufu, “hivi kama ningekuwa na hela kama zao?” au hivi kama ningekuwa maarufu kama hao? Ni mara nyingi tumejikuta tukianguka kwenye maswali “hivi kama ningekuwa….” Mbegu ndogo yaweza kuwa msitu mkubwa. Hili linafanya tujiulize swali, Je, unafikiri wewe ni mbegu ndogo sana? Inatokea katika maisha kwamba tunajisikia tupo chini na tunahitaji zaidi. Lakini haya yote hayana tofauti na ndoto zitokanazo na tamaa za dunia. Ukweli ni kwamba kila mmoja wetu ana uwezo wa kufanya mambo makubwa katika dunia hii. Machoni pa Mungu tuna hazina ndani mwetu kubwa mno kuliko yale tunayotamani sisi wenyewe.
Nini maana ya kufanywa upya na Mungu na kuwa mti mkubwa, kama punji ya haradali ilivyo? Ni kwamba kila mmoja wetu amepewa vingi na mengi ya kutimiza ili kujenga ufalme wa Mungu na mpango wa utukufu wa Mungu alionao katika maisha yetu. Ni mpango huu utakao zaa matunda makubwa na uzima wa milele. Tunaweza tusipate jina la kutambuliwa hapa duniani. Lakini, mbinguni lilo la muhimu ni utakatifu wako na jinsi ulivyo timiza mpango wa Mungu ulivyo katika maisha yako.
Alisema Mama Teresa mara nyingi kwamba “tumeitwa ili tuweze kuwa waminifu, na sio kufanikiwa.” Ni uaminifu huu kwa Mungu wenye thamani.
Sala: Bwana, ninatambua kwamba bila wewe mimi si kitu. Bila wewe maisha yangu hayana thamani. Ninaomba niweze kukumbatia mpango wako mkamilifu na wa utukufu katika maisha yangu na katika mpango huo, niweze kupata ukuu ule ulio niandalia na kuniitia mimi. Yesu, nakuamini wewe. Amina
Maoni
Ingia utoe maoni