Alhamisi. 28 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Julai 28, 2017

Ijumaa, 28 Julai, 2017,
Juma la 16 la Mwaka

Kut 20:1-17
Zab 19:8-11 (K) Yn 6:68;
Mt 13:18-18


MIZIZI ILIYOJIKITA KWA KRISTO

Injili ya leo inatualika kutafakari juu ya Yesu Kristo kama mpandaji wa neno la Mungu. Yesu anatualika tulisikilize neno la Mungu na kuongozwa nalo katika maisha yetu. Kwa kufanya hivyo mbegu iliyo pandwa mioyoni mwetu itazaa matunda. Mfano wa mpanzi unaonesha nguvu ya Neno la Mungu kwa wale wote wanao lipokea kulisikiliza na kulizamisha ndani mwao. Mfano wa mpanzi unawahusu wakristo wote hasa wale wanaopaswa kuwalisha watu neno la Mungu kama vyombo vya Kristo.

Sisi tunaona wenyewe kati yetu sisi wakristo wapo tunao jifananisha na zile mbegu zilizo anguka njiani, mbegu zilizo anguka kwenye mwamba, na mbegu zilizo pandwa katika udongo mzuri. Wakristo wote ambao hawajapandwa katika udongo mzuri ni wale ambao hawana mizizi. Wanakiri Imani ya Kristo pale tu inapo pokelewa vizuri na watu, wakati mambo ni marahisi. Lakini pale inapotoeka changamot katika kuhubiri Injili na Neno la Mungu, na wakati maisha ya kumfuata Kristo hayana umaarufu, huyu mtu huchagua njia nyingine ya tamaduni Fulani. Hili ni jambo la kweli kabisa katika maisha yetu ya sasa.Tamaduni na ulimwengu vinapingana sana na ukweli wa Imani ya Kristo. Ulimwengu unakuwa maarufu na tena wenye nguvu na kuonekana kama sehemu ya ushindi. Matatizo ya kweli yanatokana na ukosefu wa Wakristo wengi kukosa mizizi ya Imani katika maisha yao ya kila siku.

Cha muhimu kabisa ni kuruhusu hili neno la Mungu lizamishwe ndani kabisa katika udongo wa roho zetu. Hili linapo tokea neno linakuwa na kuwa imara. Na katika ulimwengu wa mawimbi tukiwa kama wakristo tutashinda mawimbi na msuko suko wa dunia. Tutafakari kama tupo tayari kusimama ndani ya Kristo au la. Tuombe Mungu azamishe mizizi ya imani katika mioyo yetu ili tuweze kuwa imara bila kujali ina tugharimu nini.

Sala: Bwana, ninatamani neno lako lizame kabisa katika moyo wangu. Ninatamani kubaki imara katika Imani yangu bila kujali gharama. Ninatamani kuwa na Imani kubwa na katika upendo wangu kwa kila kitu. Yesu, nakuamini wewe. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni