Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Agosti 06, 2016

Jumamosi, Agosti 6, 2016,
Juma la 18 la Mwaka

Sikukuu ya Kung’ara Bwana wetu

Dan 7:9-10, 13-14;
Zab 96:1-2, 5-6, 9;
2Pet 1:16-19;
Lk 9: 28-36


KUITWA KWENYE UTUKUFU!

Kuna nyakati mbili katika Kalenda ya Lirtujia tunapopata nafasi ya kutafakari juu ya tukio la Kung’ara Bwana, jumapili ya pili ya kwaresima kudhihirisha Umungu wa Kristo kabla ya mateso na kifo, na siku nyingine ni tarehe kama ya leo, tunaadhimisha kutukuka kwa utukufu wa Kristo. Zaidi ya yote Kung’ara Bwana kunaonesha ukweli wa Utatu Mtakatifu: Baba katika sauti, Mwana katika Yesu, Roho katika wingu jeupe linalo nga’ara. Mungu hapa anatupa nafasi yakuona ukuu wake katika maisha ya Utatu. Mt. Leo Mkuu anasema “Lengo kuu la Kung’ara Bwana ilikuwa ni kuondoa ndani ya mioyo ya wafuasi aibu ya Msalaba”. Kati ya mambo mengi tuangalie mambo mawili leo; la kwanza, Yesu ni Mungu kamili na mwanadamu kamili. Maisha yake na mafundisho yake hayajaletwa na mwanandamu. Maneno yake sio tuu maneno ya kawaida. Ni Mungu mwenyewe anayeongea na sisi kupitia Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo. La pili, tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na tunaitwa katika maisha ya furaha ya milele, mwili na roho mbinguni. Siku hizi katika jamii zetu tunaona wengi hawajali utu wa mwanadamu (utoaji mimba, kuua mtu kwa kumchoma sindano za dawa kwakisingizio kwamba anateseka mno bora apumzike-najiuliza unawezaje kuondoa mateso ya mtu kwa kumuua?, tunaona pia sheria za kuwanyonga watu, vita na mengine mengi). Tutambue na tusisahau kwamba mwanadamu ni kiumbe pekee duniani ambacho Mungu amependa mwenyewe kwa kumuita kushiriki, kwa njia ya akili, utashi na upendo katika maisha ya Kimungu.

Sala: Mungu Baba yetu mpendwa, tunakuomba tuige maisha ya Mwanao mpendwa Yesu Kristo yawe maisha yetu. Na hapo tutakuwa na furaha iliyo ndani yetu kama watoto wa Mungu. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni