Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Agosti 07, 2016

Jumapili, Agosti 7, 2016,
Dominika ya 19 ya Mwaka

Hek 18: 6-9;
Zab 32: 1, 12, 18-20, 22;
Ebr 11: 1-2, 8-19
Lk 12: 32-48.


KUTEMBEA NA YESU KATIKA IMANI!

Masomo ya leo yanaongelea kuhusu Imani, yakitupa mfano wa Imani ya Waisraeli, Imani ya Abrahamu na Sarah na mwishowe yakitutaka kuwa na Imani hai ndani mwetu.

Somo la kwanza kutoka kitabu cha Hekima linatuambia kuhusu Imani ya Mababu zetu waliosubiri ukombozi wa kutoka utumwani Misri. Walisubiri kwa Imani kwamba kweli Bwana atakuja kuwasaidia katika mateso yao na ukandimizwaji. Walimtukuza Mungu kwakila jambo alilowatendea, walijua yupo pamoja nao.
Katika somo la pili tunasikia kuhusu Imani na uvumilivu wa Abrahamu na Sarah mkewe, pia Isaka na Yakobo (Ebr 11:8-9). Abrahamu alimtii Mungu akaiacha nchi yake mwenyewe kwenda nchi ya ahadi. Hakuwa na shaka kwamba mke wake hata katika umri ule atapata mtoto (Ebr. 11:11). (Aliamini kwamba pamoja na kwamba yeye yupo katika umri ule bado watazaliwa watoto kutoka katika shina lake hata kama nyota wa mbinguni (Ebr. 11:12) ), alivyo ambiwa amtoe mwanaye sadaka aliamini Mungu anauwezo wakumfufua mtu na kumrudishia uhai kutoka kifo (Ebr. 11:17-19). Katika yote na vitu vyote, Abrahamu alikuwa na imani kwa Mungu, kwa uvumilivu akivumilia aone jinsi uzuri wa utukufu wa Mungu utakapokuwa na kuonekana.

Katika Injili Luka anatuambia kuwa tuwe na “uvumilivu katika imani na pia Imani iliyo hai”. Tumekombolewa na Kristo na hivyo tunapaswa kuishi maisha ya neema kila wakati, tukikwepa kuanguka kwenye dhambi. Baada ya kuwa na uvumilivu katika Imani yetu iliyo hai kwa njia ya maisha yetu, je? Tuipoteze yote kwasababu ya kishawishi kidogo? Baada ya majitoleo makubwa, je, sisi tukataliwe kuwa sehemu ya Ufalme wa Mungu kwasababu ya kuwa wavivu mwishoni? Bilashaka hapana! Hatuwezi kuchagua kutowasha taa zetu kila wakati. Hatuwezi kuchagua kulala wakati tunapaswa kuwa macho. Hatuwezi kupoteza nafasi yetu wakati tumekuwa tukivumilia mpaka sasa. Mt. Luka anaishauri jumuiya wa waaimini tusiwe baridi bali waliojawa na shauku ya Bwana.

Yesu pia anaongelea kuhusu mtumishi mwenye busara na mtumishi asiye na busara. Mtumishi mwaminifu anakimbia anaingia katika nyumba ya Bwana wake na kufanya kazi katika shamba lake. Mtumishi asiye na busara alikuwa mvivu na hakufanya kazi na kutimiza majukumu yake. Ukristo maana yake ni kuwa kama mtumishi mwenye busara, kufanya kazi yako kwa uaminifu ukitambua Mungu yupo karibu yako kila wakati. Ukristu maana yake ni kumtafuta Mungu kila wakati katika maisha yetu bila kuchoka, hakuna kupumzika Ukristo. Dhambi inatuambia Mungu hayupo karibu, kama ilivyofanya kwa Adamu na Eva. Kila Mkristu anaitwa kila mara kutambua Mungu yupo karibu kila wakati katika maisha yetu na tusikubali dhambi ituambie tofauti na hilo.

Yesu anasema, “anabahati yule mtumishi ambaye Bwana wake atamkuta akitenda kazi yake, amin nawaambia, atamchukua na kukaa chini kula na kumtumikia”. Kwa maneno haya mazuri, Yesu anatuambia kwamba wote watakao vumilia wakienenda katika Imani wamebarikiwa. Atawatumikia na kula pamoja nao katika Ufalme wa Mungu. Yesu anamalizia mafundisho yake kwakusema, “Kwa yule aliyepewa vingi, atadaiwa hata vingi zaidi”. Yesu anawatafuta wafuasi wanaojituma. Anawataka mapadre na watawa wanaojituma kwa uchungaji wa kiroho wa wana wa Mungu. Anawataka wazazi wawakuze watoto katika Imani ya Kikristo, Katoliki na katika sakramenti. Anawataka, walimu wazuri, mahakimu wazuri, wanasiasa wazuri, madaktari wazuri nk. Wote hawa katika kazi zao watahesabiwa. Imani yako katika Kristo ikufanye utende vizuri zaidi kazi yako.

Maisha ni safari ya Kiroho. Kila siku yanasonga. Abrahamu “aliishi katika hema wakati akitazamia mji atakaomuonesha Mungu, uliotengenezwa na kujengwa na Mungu”. Katika kuishi hivi, tunakuwa tayari, kwa muda wowote, kukutana na Bwana wetu na Mkombozi wetu. Na tutakapo kutana naye tutatambua yote tulioishi pamoja naye kwanjia ya wale tuliowapenda na kuwatumikia kipindi cha safari yetu.

Sala: Bwana, naomba nitembee katika njia zako siku zote za maisha yangu. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni