Alhamisi. 16 Mei. 2024

Tafakari

Jumatatu, Julai 03, 2017

Jumatatu, Julai 3, 2017,
Juma la 13 la Mwaka
Sikukuu ya Mt. Toma, Mtume

Efe 2:19-22
Zab 117:1-2;
Yn 20:24-29.


KUMSHUHUDIA KRISTO MFUFUKA!

Leo tunaadhimisha sherehe ya Mt. Tomas. Mt. Tomas anajulikana zaidi kwa swali alilomuuliza Yesu, lakini tunafarijika kwa maneno ya awali ya Yesu anapomwambia Tomaso, “Amani kwako.” Yesu hamgombezi wala kuonyesha kukasirishwa na Tomaso bali anampatia amani. Yesu anatujua jinsi tulivyo wadhaifu kwa hivyo anatupatia amani tunapokuwa tumetawaliwa na wasiwasi na woga. Ili kufikia kiwango cha kuamini Tomas haoneshi mahitaji ya kitu kingine zaidi ya kile ambacho tayari wenzake walikipata. Anachosema Tomaso ni kwamba yeye pia anataka nafasi ya kushuhudia kwa nafsi yake – kama ilivyokuwa kwa kila mmoja wao – ili aweze kuamini habari hiyo ya kushangaza. Lakini jambo hilo haliishii hapo kwa kuwa mwinjili Yohane au Yesu mwenyewe anasema “umeamini kwa sababu umeniona, wana heri wale wasiona wakasadiki.” kwetu sisi kipengele hiki ni muhimu zaidi. Tutaamini vipi wakati hatujaona? Tomaso hakuamini mpaka alipoona. Petro hakuweza kuamini mpaka alipoona. Maria Magdalena naye pia hakuamini mpaka alipoona. Sisi tutaamini vipi wakati hatujaona? Hii inawezekana kwa sababu tumebarikiwa “Heri wasiona wakasadiki.” Kwa hiyo tunalazimika kutambua kuwa imani yetu hatujaipata kwa uwezo wetu au kwa dini yetu bali ni zawadi toka kwa Mungu. Japokuwa hatujamwona kwa macho yetu huyu Yesu mfufuka Mungu aliyejaa wema na ukarimu ametupatia kichocheo cha imani kwa Kristo mfufuka.


Sala: Bwana wangu imarisha imani yangu kama Tomaso aliyesema “Bwana wangu na Mungu wangu.” Yesu nakutumainia wewe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni