Alhamisi. 16 Mei. 2024

Tafakari

Jumamosi, Julai 01, 2017

Jumamosi, Julai 1, 2017.
Juma la 12 la Mwaka

Kumbukumbu ya Bikira Maria

Mwa 18: 1-15;
Lk 1: 46-50, 53-55;
Mt 8: 5-17


IMANI YA JEMEDARI

Masomo ya leo yanatuletea aina ya hali mbili zinazo pingana. Wakati, Abrahamu anamuomba Bwana (katika hali ya watu watatu) kuingia katika hema yake, Jemedari katika Injili anamsihi Yesu asiingie nyumbani kwake. Wakati mke wa Abraham, yaani Sarah anakosa Imani, Jemedari anamwamini Yesu kwa Imani ya hali ya juu sana.

Huyu Jemedari ambaye alikuwa mpagani, alikuja kwa Yesu kwa nia ya mtumishi wake aponywe. Alitambua kuwa Yesu ana nguvu ya kuamuru kila kitu, kama yeye alivyo na uwezo wa kuamuru watumishi wake waliokuwa chini yake. Aliamini kwamba ilitosha kabisa kwa Yesu kusema neno tu, hata bila kutembelea nyumba yake. “Bwana, sistahili uingie kwangu, sema neno tu na mtumishi wangu atapona (Mt 8:8)”. Maneno haya tunayarudia kila siku wakati wa misa kabla hatuja pokea komunyo. Ni maneno ya unyenyekevu mkubwa na Imani kuu kutoka kwa huyu Jemedari wa Kirumi aliye muomba Yesu amponye mtumishi wake kutoka mbali. Yesu anavutiwa na Imani ya huyu mtu na anasema “katika Israeli sijawahi kuona imani kubwa namna hii”.

Jemedari anakubali kwamba “hastahili” Yesu aingie katika nyumba yake. Hakuna hata mmoja wetu anayestahili Yesu aingia kwake na kupokea neema kubwa namna hii. Hatustahili Yesu kuja ndani ya mioyo yetu nakufanya maskani yake. Katika hali ya utambuzi ya unyenyekevu mkubwa, tunaweza kukubali kwamba Yesu ameamua kuja kwetu. Huyu Jemedari alistahilishwa na Yesu kwasababu Mungu alimpa neema yake kwasababu ya kuwa na unyenyekevu mkubwa.

Na ukweli kwamba huyu Jemedari alitambua kuwa hastahili kupata neema ila ilimfanya Imani yake iwe takatifu zaidi. Hii ina maana kwamba Imani yetu kwa Yesu haipaswi kujikita katika hali ya kwamba tuna haki ya uwepo wake katika maisha yetu, bali, ioneshe kwamba Imani yetu imejikita katika kukubali kwa akili zetu kuhusu huruma yake isio na mwisho. Tukiona huruma hio, tutakuwa katika hali ya kuitafuta. Kwani Yesu anapenda tutafute huruma yake licha ya kutokustahili kwetu.

Tuombe kuwa na Imani kama ile ya hule Jemedari,. Tumwache yeye awe mfano wetu hasa wakati Yesu “anapo ingia nyumbani kwetu” tunapo enda kumpokea katika komunyo takatifu kila wakati.

Sala: Bwana, sistahili. Sistahili hasa kukupokea katika komunyo takatifu. Nisaidie mimi nitambue ukweli huu kwa unyenyekevu, nisaidie niweze kutambua ukweli kwamba unatamani kuja kwangu. Yesu, nakuamini wewe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni