Alhamisi. 16 Mei. 2024

Tafakari

Jumatatu, Juni 26, 2017

Jumatatu, Juni 26, 2017.
Juma la 12 la Mwaka

Mw 12: 1-9;
Zab 33: 12-13, 18-20, 22;
Mt 7: 1-5.

USIHUKUMU!

Kuwa mtu wa kuhukumu inaweza kuwa jambo ngumu kuliacha. Mmoja anapo jiingiza katika tabia ya kuhukumu daima na kufikiria na kuongea kwa ukali na hali ya upinzani, ni vigumu kwa watu kama hao kubadilika. Ni hakika, mmoja anapo jiingiza katika njia ya kupinga na kuhukumu, nafasi ya kubakia katika njia hiyo ya kupinga na kuhukumu yaweza kuwa kubwa na huenda akaendelea kuwa hivyo kadri siku zinavyo sogea. Hii ndio maana Yesu anakataza jambo hili kwa nguvu kabisa. Baada ya maneno hayo Yesu alisema “Enyi wanafiki, ondoa kwanza kibanzi ndani ya jicho lako kwanza... “ maneno haya ya Yesu na hali yake ya kukataza hali hiyo ya kuhukumu sio kwamba Yesu ana hasira au ni mkali juu ya watu wanao hukumu. Bali, anataka kuwaelekeza njia sahihi, kutoka katika njia mbaya na kuwaweka huru kutoka katika mzigo huu mkubwa. Kwa hiyo swali muhimu la kujiuliza ni hili “Je, Yesu anaongea na mimi?” je, ninateseka kwasababu nimekuwa mtu wa kuhukumu wengine daima? Kama jibu ni ndio wala usiogope wala kukata tamaa. Kuona hali hii na kuikiri ni muhimu sana na ni hatua ya kwanza ya fadhila ambayo huenda kinyume na hali ya kuhukumu. Fadhila hii ni huruma. Na huruma ni kati ya fadhila kubwa tunayo paswa kuwa nayo leo hii.

Inaoneka muda tunaoishi sasa tunahitaji huruma zaidi kuliko kipindi kingine chote. Pengine moja ya sababu ya hiyo, ni hali ya juu ya tamaduni za dunia zimekuwa kali sana juu ya watu. Unacho paswa kufanya ni kusoma magazeti, angalia mitandao ya kijamii au angalia habari mbali mbali za ulimwengu utatambua kuwa utamaduni wa dunia unakuwa katika hali ya kutangaza dhambi za watu. Tatizo lipo. Kizuri kuhusu huruma, Mungu anatumia hali yetu ya kuhukumu au hali yetu ya kuhurumia na kusamehe kama njia ya kutuhudumia sisi. Yeye ataonesha huruma kubwa na msamaha kwetu kama tutawaonesha fadhila hii. Lakini pia atatumia pia haki yake na hukumu kama tutaamua kuchukua njia hiyo. Ni juu yetu!

Washiriki wa ufalme wa Mungu wanapaswa kuacha hukumu kwa mwenye mamlaka nayo (Mungu). Kama Bwana wao wanapaswa kuwa watu wakuponya na kuonesha huruma. Dhamiri iwe, kumpenda jirani yangu kama nafsi yangu. Na pia hatujui wala kufahamu ukweli kuhusu mtu. Hakuna mwanadamu aliye mwema kabisa mwenye haki au uwezo wa kumuhukumu mwanadamu mwenzake. Kuna usemi mzuri wa kichina unaosema “Tunaona kidogo sana kilichopo mbele ya macho yetu, sehemu kubwa ipo nyuma ya macho yetu”

Tafakari leo, je, hali yako ya kwanza ni ipi? Jikumbushe mwenyewe kwamba huruma inalipa zaidi kuliko kuwa mtu wa kuhukumu. Huruma huleta uhuru na furaha. Weka huruma katika akili yako na tazamia zawadi zinazo tokana na fadhila hii ya thamani kubwa.

Sala: Bwana, jaza moyo wangu kwa huruma yako. Nisaidie niweze kuachana na hali ya hasira na hali ya kuwahukumu wengine. Badilisha hali hiyo kwa upendo wako. Nisaidie nitazame maisha yangu kwanza, kabla sija saidia wengine wabadilike. Yesu, nakuamini wewe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni